Nani kasema watoto wetu wapo salama? Kila kona sasa ni hatari, wakati kesi ya kumkata kichwa mtoto inayomkabili Ramadhani na Mamaye ikipigwa kalenda na maalbino wakiishi maisha ya hofu kote nchini, mauaji ya watoto yamebisha hodi Dar es Salaam na mmoja amenyongwa mchana kweupe. Ema Mapunda, mama wa mtoto mchanga wa mwezi mmoja na siku mbili, jana alijikuta katika majonzi makubwa baada ya kukuta mwanaye, Jonathan Chale, ameuawa kikatili eneo la Mbezi Temboni, jijini Dar es Salaam. Tukio hilo la kusikitisha na kuzidisha hofu kwa wazazi wenye watoto wadogo, lilitokea jana majira ya saa tatu asubuhi wakati mama huyo alipokwenda kuchota maji kisimani na kuacha kichanga hicho kitandani. Uchunguzi wa awali wa kipolisi unaonyesha kwamba kichanga hicho kimeuawa kikatili kwa kunyongwa hadi kufa kisha kukatwa ulimi na mtu asiyefahamika. Nipashe ilishuhudia mwili wa kichanga hicho ukiwa umefukiwa na sehemu ya kichwa ikiwa nje. Mjumbe wa shina namba 45 Mbezi Temboni, Iddie Gereza, akisimulia tukio lilivyokuwa alisema kuwa mama mwenye mtoto huyo alikwenda kuchota maji. Mama huyo akiwa huko kisimani mara alisikia sauti ya mtoto akilia na aliporejea nyumbani alikuta mtoto hayupo kitandani. ``Kwa sababu mama huyo alimwacha mtoto kitandani kalala alidhani kuwa analia kutokana na kuachwa mwenyewe chumbani ama kakojoa au jambo lolote linaloweza kumfanya aliye, hivyo hakuwa na hisia zozote mbaya,`` alisema Gereza. Baada ya mama huyo kusikia kelele zinazidi aliamua kuharakisha kuchota maji kisha akarudi nyumbani, lakini alipokaribia kuingia ndani hakusikia tena sauti ya mtoto akilia. Mama huyo ambaye alifika Dar es Salaam akitokea Songea miezi kadhaa akiwa mjamzito, alipigwa na mshangao baada ya kufika chumbani alipomwacha mtoto huyo na hakumkuta. ``Alichofanya mama huyo ni kutoka nje na kupiga makelele kuomba msaada wa watu ambapo majirani tulijitokeza na kuanza kutafuta kama kuna mtu aliyepita akiwa kabeba mtoto huyo,`` alisema Gereza. Mjumbe huyo alisema kuwa baada ya kutawanyika kwa dakika 10 au 15 walirejea tena kwene nyumba ya mama huyo na kuanza kujipanga wafanyeje baada ya kutoona mtu yeyote akiwa na mtoto. Wakiwa hapo nyumbani, mtu mmoja alitoa ushauri kuwa kwanini wasijaribu kutafuta katika pori ambalo lipo jirani na nyumba hiyo. ``Wazo hilo tuliliona kuwa ni zuri na hivyo tukaamua kufanya hivyo tukiwa tunatafuta katika kijipori hicho tulioa majani yanachezacheza mbele yetu na tuliposogela karibu tuliona paka mkubwa akikimbia,`` alisema Gereza. Aliongeza kuwa baada ya paka kukimbia karibu na sehemu aliyokuwa amesisimama palikuwa pametifuliwa kama vile kuna kitu kimechimbiwa chini. Alisema Baada ya kuona hali kama hiyo waliamua kukata mti na kupachimbua ndipo walipokuta kuna mtoto kafukiwa. ``Tulivyoona hivyo tukamwita yule mama na kumuuliza kama mtoto huyo ni wake, alipomuona tu akaanguka na kuzimia pale pale,`` alisema Gereza. Alisema baada ya hapo wakapiga simu polisi ambapo walikuja ndani ya dakika 45 na kuthibitisha tukio hilo ambapo walitakiwa kwenda polisi kutoa maelezo zaidi. Uchunguzi wa awali uliofanywa na polisi umebaini kuwa tukio hilo litakuwa limefanywa na mwanamke kutokana aina ya nyayo zilizoonekana zikielekea sehemu uliokutwa mwili wa mtoto huyo. Baadaye majira ya saa 8:45 mchana polisi walikuja wakiwa wamefuatana na mama wa marehemu, mjomba wa mama wa marehemu anayeitwa,Thomas Komba, kuja kufukua mwili huo. Polisi hao walikuja na gari ania ya Land Cruser PT 1412 na kuufukua mwili ambapo waliukuta umekatwa ulimi sambamba na kuwepo kwa haja kubwa pembeni kuonyesha kuwa alikufa kwa kunyongwa. Mwili huo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala, jijini Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Marc Karunguyeye, jana alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa sasa polisi inalifanyia uchuguzi kujua chanzo chake. ``Tumepewa taarifa za kuwepo kwa tukio hilo ambapo huyo mama alikwenda kuchota maji na aliporudi hakumkuta mwanaye hivyo tunayafanyia uchunguzi maelezo yake,`` alisema Karunguyeye. Hata hivyo, habari kutoka Gereza zinasema kwamba mama huyo wa marehemu alikuwa amekatiwa tiketi ya kurejea Songea leo. Nipashe ilipowasiliana na mjomba wa mama wa marehemu, Thomas Komba alisema kwamba tukio hilo limeishangaza familia na hawajui jinsi lilivyotokea. `` Kwa sasa niko hapa polisi Mbezi, mpaka sasa hivi hatujui hili tukio lilivyotokea, sisi tunaona kama sinema,`` alisema. Komba alisema kwamba leo mama wa marehemu alikuwa amepanga kurudi kwa mumewe Songea. ``Hana matatizo yoyote na mumewe, pia hapa Dar es Salaam alikuwa na watoto wake wawili, alikuja kwangu na bahati nzuri akajifungua hapa, nikamwambia kaa kwanza upate nguvu ili uweze kurejea Songea,`` alisema.
SOURCE: Nipashe
No comments:
Post a Comment