WAZIRI Mkuu Mstaafu Joseph Warioba amezungumzia suala la ufisadi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kuonya kwamba endapo wamiliki wa Kampuni ya Kagoda hawatafikishwa mahakamani EPA itaendelea kuisumbua serikali.
Warioba aliiambia Mwananchi Jumapli kwa njia ya maandishi kuwa ni wazi kwamba Kagoda ni moja ya kampuni ambazo zimejitokeza kurejesha fedha hizo, hivyo wamiliki wake wanajulikana.
"Fedha zilizorudishwa ni bilioni zaidi ya 60. Naamini ni utaratibu tu unafuatwa na siku moja wamiliki wa Kagoda watafikishwa mahakamani. Wasipofikishwa mahakamani EPA itaendelea kusumbua taifa," alisema.
Alisema mambo mengi yameripotiwa na vyombo vya habari kuhusu makampuni yaliyohusika na kuchota fedha za EPA na ambayo wanaohusika hawajafikishwa mahakamani, hasa kampuni ya Kagoda, lakini anaamini kuwa subira inahitajika.
Warioba ambaye alikuwa akijibu swali aliloulizwa ana maoni gani kuhusu vita dhidi ya ufisadi inayoendeshwa nchini hivi sasa, alisema chimbuko la kesi za EPA ni Kampuni ya Kagoda na kwamba ukaguzi wa kwanza uliofanywa na kampuni ya Deloitte and Touche ulihusu ka mpuni hiyo.
Ukaguzi ulikuwa makini na ndio uliozaa ukaguzi wa pili wa Ernest and Young. Kati ya sh bilioni 90 zilizochukuliwa na makampuni yaliyoghushi, Sh bilioni 40 zilichukuliwa na Kagoda.
Hata hivyo, alisema jitihada kubwa zimefanywa na serikali kupambana na ufisadi, siku za nyuma watu wadogo ndio waliokuwa wanafikishwa mahakamani, lakini hatua ya sasa ya kuwafikisha mahakamani watu wazito inatia matumaini makubwa.
Alisema kesi zote zilizo mahakamani zimetokana na msukumo wa kisiasa, sio matokeo ya kazi za kawaida za taasisi ya kupambana na uhalifu kama vile Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru).
No comments:
Post a Comment