.

.

.

.

Wednesday, March 04, 2009

KANDA BONGOMAN KUTUMBUIZA NEW MSASANI CLUB


MWANAMUZIKI mahiri wa muziki wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kanda Bongoman anatarajia kuwasili leo nchini kwa onyesho maalum litakalofanyika kesho katika ukumbi wa New Msasani Club jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Kampuni ya Victoria Entertainment ya jijini Dar es Salaam, Mathar Baluhi alisema mwanamuziki huyo atawasili leo saa 9.00 alasiri kwa ndege ya Shirika la KLM.
Kama tunavyomfahamu huyu (Bongoman) aliwahi kutamba na vibao kama Sayi, Isambe, Monie, Nzinzoo, Lize na Muchana na vingine vingi ambapo mpaka sasa nyimbo zake zikipigwa bado zinapendwa kutokana na umahiri wake wa kucheza na kuimba, alisema Baluhi.
Baluhi alisema kuwa onyesho hilo litasindikizwa na Bendi ya FM Academia Wazee wa Ngwasumaí na linategemewa kuwa la aina yake kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika.
Sisi tumeshirikiana na wenzetu NY Production kumleta Bongoman nchini kwa hiyo wapenzi wa muziki wa dansi wajitokeze kwa wingi ili kupata burudani kwani mwanamuziki huyu ni mmoja kati ya wasanii wanaotamba barani Afrika, alisema Baluhi na kuongeza:
Tumepanga kuwa na kiingilio cha Sh 10,000 kwa viti vya kawaida na 30,000 kwa viti maalum, onyesho hilo litaanza saa tatu usiku."
Alisema wao wameamua kumleta nchini mwanamuziki huyo ili kutoa burudani kwa wapenzi wa muziki wa dansi wa rika zote kutokana na maonyesho mengi nchini kwa siku za karibuni kuwa yale yanayofanywa na vijana hasa wa muziki wa kizazi kipya, maarufu Bongo fleva.
Onyesho hilo litakuwa na watu wa rika zote kutokana na kuwepo pia kwa bendi ya FM Academia. Lakini, pia kutakuwa na watu wa makamo na wazee ambao wangependa kujikumbusha muziki wa Bongoman ambaye bado nyimbo zake zinatamba na kupendwa licha ya kuwa alizipiga zamani, alisema Baluhi
Ujio wa Bongoman ambaye pia ni mahiri kwa mitindo ya mavazi unafanyika miezi michache baada ya mwanamuziki mwingine wa Kikongo, Mbilia Bel na rapa Fally Ipupa kutumbuiza katika ukumbi wa New World Cinema, Mwenge jijini Dar es Salaam na kukonga roho za mashabiki wengi wa muziki wa dansi.

No comments:

Post a Comment