Rais Jakaya Kikwete amesema ana orodha ya majina ya wafanyakazi wa kampuni ya ukaguzi na ukadiriaji wa mizigo ya TISCAN, wanaoshirikiana na wafanyabiashara kukwepa mizigo yao kukaguliwa na kuamuru wafanyakazi hao wafukuzwe kazi mara atakapokabidhi majina hayo. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo leo alipofanya ziara ya ghafla katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), ambapo alisema orodha hiyo anaifanyia kazi. “Majina hayo sasa nayafanyia kazi, waambie watu wa Maktaba (makao makuu ya kampuni hiyo) mtindo wanaofanya unajulikana, sitawaumbua hadharani, majina yao nitawapa wakubwa zao na nikiwapa tu watoeni kwenye kazi,” alisema. Rais Kikwete alisema wafanyakazi hao wamekuwa na tabia ya kushirikiana na wafanyabiashara na kuwapa mbinu za kufanya, ili mizigo yao inayoingia nchini, isiweze kupitishwa kwenye mashine ya ukaguzi inayotumia mionzi, hivyo kutozwa kodi ndogo.
“Tiscan pale maktaba kwa kutumia simu, mfanyakazi anamfundisha mtu aliyepo Dubai (Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE) namna ya kujaza fomu na kontena lake linapoingia nchini, lionekane amebeba mtumba asipitishwe kwenye skana kumbe ndani kuna VX… nikiwa Ikulu naelezwa kila kitu, hii ndiyo Bongoland, nasi tuongeze bongo, wao wanatajirika tu, watoeni kwenye kazi,” alisema.
Mbali na hilo, Rais Kikwete aliagiza TPA kununua eneo la Kampuni ya Wakala wa Meli (NASACO) lililopo ndani ya eneo la bandari hiyo kwa ajili ya kuhifadhi kontena. Eneo hilo la Nasaco, lipo chini ya mufilisi kutokana na kesi inayoendelea mahakamani, iliyosababishwa na deni la mamilioni ya shilingi ambayo kampuni hiyo inadaiwa na watu mbalimbali, hali ambayo Rais Kikwete aliitaka TPA kuwaomba kuzungumza nao nje ya mahakama na kuwalipa deni hilo, ili waweze kulimiliki wao. Rais Kikwete aliihimiza mamlaka hiyo kufanya kazi kwa lengo la kuleta ufanisi na kuwaeleza kuwa wakati wowote atafanya ziara ya kushitukiza kabla ya mwisho wa mwezi ujao, kuona kama wameongeza ufanisi kama walivyoahidi. Awali Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Ephraim Mgawe, alisema tangu Januari 26 hadi juzi, idadi ya meli zilizokwishapakua mizigo zimepungua kutoka 23 hadi 16. Akifafanua, alisema meli za kontena zilikuwa 12 sasa 14, meli za mafuta kutoka nne hadi mbili na meli zilizokuwa na mizigo kiujumla kutoka saba na hadi juzi kulikuwa hakuna hata moja. Mgawe alisema muda wa meli kusubiri nje kupakuliwa umepungua kutoka wastani wa siku tisa hadi sita ambapo lengo ni kufikia wastani wa kati ya siku mbili na siku moja ifikapo mwezi ujao. Alisema chombo cha kupakulia mizigo cha kampuni ya kupakia na kupakua kontena (TICTS) kilichoharibika kwa kipindi cha mwaka mmoja, kilianza kufanya kazi juzi na kuongeza, “tumepata vyombo vipya vya kupakulia kontena vinne, tutawakodisha Ticts viwili kwa lazima, hivyo vyombo vya kupakulia vitakuwa tisa”. Alisema kati ya Januari 26 hadi juzi, idadi ya kontena zilizopo bandarini imepungua kutoka 10,500 hadi 7,796. Kwa siku kontena 200 hadi 300 hupakuliwa na Ticts wakati zinazoingia ni 1,000 kwa siku. Rais Kikwete aliwataka kuhakikisha kontena zinapakuliwa ndani ya siku saba na zisikae muda mrefu bandarini, ambapo wenye kontena wamegeuza eneo la bandari kama sehemu ya kuhifadhi mizigo yao.
No comments:
Post a Comment