.
.
Sunday, March 01, 2009
UHABA WA UMEME NJIANI TANZANIA
Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), limetahadharisha nchi inahitaji umeme wa dharura hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe kununua mitambo ya Dowans haraka. Tayari serikali imepingwa vikali na wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, katika suala zima la kutaka kununua mitambo ya kampuni hiyo. Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idrisa Rashid, iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana ilieleza kuwa utafiti wa ukuaji wa sekta ya umeme nchini unaonyesha mahitaji ya nishati hiyo yanaongezeka kwa kasi na katika kipindi cha mwaka huu na 2013 kutakuwa na uhaba mkubwa wa umeme. Katika taarifa hiyo, Dk. Rashid alisema kutokana na kasi ya ongezeko hilo, kuna umuhimu wa kuwa na mashine kubwa kwa ajili ya kukabiliana na dharura itakayojitokeza. ``Kwa sasa mahitaji ya umeme yamefikia megawati 700 na gridi ya taifa haina ziada yoyote hii ina maana kuwa zaidi ya megawati 105 zinahitajika kuongezwa kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya umeme katika kipindi hicho ukilinganisha na ukuaji wa mahitaji ya umeme, ambayo ni asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka,`` alisema Dk. Rashid katika taarifa hiyo. Alisema tayari shirika lilishafanya ukaguzi katika mitambo ya Dowans na kubaini kuwa ipo katika hali nzuri.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment