.

.

.

.

Friday, March 06, 2009

WAKAMATWA NA VIUNGO VYA BINADAMU


Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza, Jamal Rwambow akionyesha mifupa ambayo inasadikiwa kuwa ya ALBINO.
Watu watano wakiwemo waganga wawili wa jadi, wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kukutwa na viungo vya binadamu mkoani Mwanza. Tukio hilo limekuja ikiwa zimebaki siku nne wakazi wa Kanda ya Ziwa wapige kura za maoni kuwataja watu wanaowashuku kujihusisha na mauaji ya albino.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jamal Rwambow,alisema watu hao walikamatwa jana wakiwa na viungo vya binadamu
Kamanda Rwambow alivitaja viungo hivyo kuwa ni pamoja na mifupa ya bega pamoja na mbavu.
Hata hivyo, alisema viungo hivyo bado haijafahamika kama ni vya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) au la. Alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 8:00 mchana katika Wilaya ya Nyamagana, jijini Mwanza.
Aliwataja wanaoshikiliwa kuwa ni pamoja na Joseph Baso (32) mwenyeji wa Kinampanda mkoani Singida, Hellena Maulid (42) mkazi wa Musoma, George Mohamed (39) wa Nyakato, mkoani Mwanza, Francis Pastory (41) mkazi wa Kayenze na Msombo Amule (58) mvuvi, wote waganga wa kienyeji wakazi wa mkoani Mwanza
Kamanda Rwambow alisema ushirikiano wa wananchi na polisi, ndiyo uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao pamoja na viungo hivyo.
Alisema hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao baada ya upelelezi kukamilika. Kamanda Rwambow alisema Mkemia Mkuu wa Serikali, atahusishwa katika kutambua aina ya binadamu mwenye viungo hivyo pamoja na umri wake
Aidha, Kamanda Rwambow amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika mwendelezo wa kuwasaka watu wanaojihusisha na vitendo vya mauaji ya maalbino na vikongwe kutokana na imani za kishirikina.

No comments:

Post a Comment