.

.

.

.

Monday, March 02, 2009

MACHIFU WATOA OMBI LAO KWA SERIKALI

WAZEE wa mila (machifu) wa makabila ya Wilaya ya Mbeya wameiomba serikali iwape ruhusa ya kutumia 'darubini' zao ili kuweza kuwakamata wauaji wa maalbino, wapiga nondo na kuwahamishia "mimba wanaume wanaowapa mimba "wanafunzi ili kukomesha tabia hizo.
Waliyasema hayo jana katika mkutano na mkuu wa mkoa uliohudhuriwa na machifu zaidi ya 100 kutoka Wilaya ya Mbeya Vijijini na jiji katika ukumbi wa shule ya sekondari ya Igawilo Uyole nje kidogo ya Jiji la Mbeya.
Walisema kuwa wanashangazwa na tabia ya serikali kutowashirikisha viongozi hao katika matukio mbalimbali yakiwemo ya uhalifu, ya kuwasaka wauaji wa watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), upigaji nondo ambao umekithiri mkoani hapa na watu wanaowapa mimba wanafunzi na kuwaharibia maisha.
Mwenyekiti wa wazee wa mila wa wilaya, Shayo Masoko (chifu mkuu ) alisema kuwa wameamua kuandaa mkutano huo na kumwita Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile baada ya kuona kumekuwepo na ongezeko la matukio ambayo hayaipendezi jamii na serikali imekuwa ikifanya jitihada zake kwa kutumia gharama kubwa bila mafanikio.
"Sisi mkuu wa mkoa tumekuita hapa tunataka tuongee na wewe kwa niaba ya serikali yetu, kwani kumekuwa na matukio mengi mabaya, lakini nyinyi kama serikali mmekuwa hamtushirikishi sisi wazee wa kimila sijui kama mnatudharau au hamtambui kama tuna uwezo mkubwa ambao tumepewa na Mungu wa kuweza kuyamaliza matatizo hayo,"alisema.
Chifu Masoko alisema kuwa machifu hao wana uwezo mkubwa wa kukomesha matukio hayo kama serikali itawashirikisha na kuwapa ruhusa ya kukemea na kutumia 'darubuni' zao kwani wazee hao wana kamati zao za ufundi ambazo wamepewa na Mwenyezi Mungu.
"Tumelisikia tukio la hawa ndugu zetu maalbino sisi tuna uwezo wa kuhakikisha wanakamatwa wahalifu wote na hawa wapiga nondo pia hawatushindi, kwa kupitia 'darubini' zetu tunaweza kusababisha wakamatwe au kuwavunja vunja miguu ili kukomesha matukio hayo."
Alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuisaidia serikali katika masuala kama hayo zaidi ya machifu, hivyo ni vema serikali ikachukua hatua za haraka katika kuwaruhusu ili waweze kutumia 'darubini' zao na sauti zao ili kuweza kukomesha tabia hiyo na serikali isiingie gharama kubwa katika kutafuta wahalifu hao.
Naye chifu mkuu wa Tarafa ya Tembela Wilaya ya Mbeya Vijijini, Rocket Mwanshinga alisema kuwa hata kwa wale wanaume wanaowapa mimba wanafunzi mashuleni, machifu hao wana uwezo wa kuwahamishia mimba hizo ili iwe fundisho kwa wanaume wengine na kupunguza tatizo la mimba mashuleni.
Alisema kuwa kama machifu wanasikitishwa na ongezeko la wanafunzi kupata mimba wakiwa shuleni na baadaye wanaume wanaowapa mimba huwakataa na maisha ya watoto hao kuharibika, hivyo dawa ni mimba hizo kuzihamishia kwa wanaume hao ili iwe fundisho kwa wanaume wengine .

No comments:

Post a Comment