WATU watatu wamekufa na wengine saba kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugongwa na kukandamizwa na lori lililobeba kokoto. Gari hilo la abiria lilikuwa limeegeshwa kwenye kituo cha basi cha Kwa Mathias, mjini Kibaha. Lori hilo lililokuwa likitokea Msoga, Chalinze lilipamia gari la abiria aina ya Toyota Hiace lililokuwa likishusha abiria, baada ya dereva kushindwa kulimudu kutokana na mwendo kasi. Baada ya Hiace kugongwa, iliburuzwa umbali wa mita 10 na baadaye kutumbukia kwenye mtaro, ambapo lori lilifuata juu. Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Absalom Mwakyoma, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo. Mwakyoma alisema ilihusisha lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 873 AAN, mali ya Kampuni ya STDAG ya mjini Dar es Salaam, likiendeshwa na Juma Sufiani (49). Alisema Hiace ilikuwa ikiendeshwa na Heniel Mfinanga (35), ambaye amevunjika mikono. Kamanda Mwakyoma alisema ajali hiyo ilitokea saa 2.40 asubuhi, ambapo lori hilo likiwa mwendo kasi liliyumba baada ya kupita kwenye tuta. Alisema Haice hiyo iliyokuwa inapakia abiria kituoni ilikuwa na watu tisa ndani, ambapo waliokufa ni Ramadhan Omary, ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Bundikani, iliyoko Mailimoja; Athuman Juma na mwingine ambaye hajatambuliwa. Majeruhi wa ajali hiyo ni Venose Liseki (32), mkazi wa Kinondoni, Hassan Ngoma, Athuman Jumanne na mwingine ambaye hajatambuliwa, ambao walipelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana hali zao kuwa mbaya. Wengine ni Charles Henry (30), Kambi Omary (20), mkazi wa Msangani, Kibaha na Mfinanga, ambao wamelazwa katika hospitali ya Tumbi. Kamanda Mwakyoma alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori, aliyekuwa kwenye mwendo kasi. Dereva huyo anashikiliwa na polisi. 000
No comments:
Post a Comment