.

.

.

.

Monday, June 07, 2010

BRAZIL NA TANZANIA KUKIPIGA UWANJA WA TAIFA JIONI HII


Leo kuanzia saa 12:00 jioni, timu ya taifa ya soka ya Brazil itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kucheza dhidi ya wenyeji wao, timu yetu ya taifa ya soka, Taifa Stars.

Sisi tunaona mechi hii dhidi ya Brazili, ambayo ilitarajiwa kutua nchini jana usiku ikiwa na nyota wake wote 23 na maafisa 37 wa benchi la ufundi, ni fursa ya aina yake kwetu.

Ni kwa sababu historia haionyeshi kwamba hapo kabla, nchi yetu iliwahi kupata bahati kama hii ya kutembelewa na timu ya taifa lolote lililowahi kubeba Kombe la Dunia.

Sisi tunaona kwamba mechi yetu hii dhidi ya Brazil, ni matokeo ya bahati tusiyoitarajia. Ukweli ni kwamba wababe hawa waliotwaa ubingwa wa dunia mara nyingi zaidi katika historia ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa michuano hiyo hawapatikani kirahisi, hasa katika nchi zilizo nyuma kisoka kama yetu.

Tunaona kuwa ni bahati ya mtende kuota jangwani kucheza dhidi ya Brazili kwa sababu ukilinganisha kiwango chao na chetu, hutakosea kuamini kwamba ni kama usiku na mchana. Viwango vipya vya ubora vilivyotolewa na Shirikisho la Soka la Kimataifa, (FIFA), vinaonyesha kwamba Brazil wanakamata nafasi ya kwanza kwa ubora, il-hali Tanzania yetu inashika nafasi ya 109. Ni tofauti kubwa sana.

Lakini, kwa namna isiyotarajiwa, nasi Watanzania tutakuwa na fursa ya kuwaona ana kwa ana wachezaji wote nyota wa Brazili kwa sasa, wakiwemo Kaka wa klabu ya Real Madrid ya Hispania, Robinho wa Santos ya Brazil, Maicon na Lucio wa mabingwa wa Ulaya, Inter Milan ya Italia na Dani Alves wa mabingwa wa Hispania, Barcelona. Orodha yao ni ndefu.

Sisi tunaamini kwamba hata mashabiki wa soka nchini, hawatatofautiana na sisi katika kukiri kwamba ujio wa Brazili ni bahati ya pekee, ni fursa ambayo hapo kabla hakuna aliyeiwazia. Hongera kwa waliofanikisha mipango ya ujio wao.

Hata hivyo, wakati sote tukiifurahia ziara ya Brazili inayosaka rekodi ya kutwaa ubingwa wa sita wa dunia na pia kuwa nchi ya kwanza kubeba kombe la michuano hiyo katika ardhi ya Afrika, kuna haja ya kuwakumbusha Watanzania wote, na hasa wachezaji wetu, kwamba tusiishie kuchekelea tu.

La muhimu zaidi kuzingatia, ni kuendeleza ukarimu wetu ili Brazili wenye mashabiki katika kila kona ya dunia wasituletee sifa mbaya pindi wakikumbana na yale yasiyoyatarajiwa.

Wachezaji wetu pia wajifunze moja kwa moja katika kila zuri walilo nalo wageni hawa wa kihistoria. Wahakikishe kwamba wananufaika na umahiri wa Brazili ili siku moja, nasi tuwe na uwezo wa kutandaza soka la kiwango cha kimataifa.

Wachezaji wetu watambue kwamba wakati wakiwa uwanjani kucheza na nyota hao, watu wengi duniani watakuwa wakiifuatilia mechi hiyo na hivyo ni fursa nyingine kwao kujitengenezea mazingira ya kupata ‘ofa’ za kusajiliwa na klabu kubwa za nje ya Tanzania na Afrika.

Mbali na kupata nafasi hiyo adhimu, sisi tunaona kwamba wachezaji wa Stars wanapaswa kucheza kwa umakini mkubwa, wakionyesha soka safi na kuwafunga magoli wageni hao kadri itakavyowezekana.

Hata hivyo, tunawakumbusha vilevile kwamba, wajaribu kuepuka faulo za kizembe, zitakazowadhuru wenzao wanaokuja kucheza kirafiki na si kimashindano.

Kamwe halitakuwa jambo zuri kuona kwamba mchezaji wetu mmoja, amecheza faulo ya makusudi kumjeruhi nyota kama Kaka na kumkosesha Kombe la Dunia litakaloanza kushindaniwa Juni 11, Ijumaa. Hilo hatulitarajii.

Sisi, pengine na Watanzania walio wengi, tutafurahi kuona nyota wetu kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakicheza soka la kuvutia kiasi cha kuushangaza ulimwengu, wakiwapiga chenga za maudhi waasisi hao wa soka linalosisimua la mtindo wa ‘samba’ na kuwakimbiza kuanzia mwanzo wa mechi hadi mwisho.

Kila la heri Stars. Tunawatakia mafanikio mema katika ‘mechi darasa’ yenu ya leo, nasi tutawashangilia kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho.

No comments:

Post a Comment