SHIRIKA la Ndege la Uturuki, Turkish Airlines linataka kuutumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dar es Salaam (JNIA) kama kitovu chake cha biashara katika Ukanda wa Mashariki na Kati Afrika, imeelezwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya shirika hilo kuzindua safari zake za moja kwa moja za kutoka Istanbul, Uturuki hadi Dar es Salaam zitakazokuwa mara tatu kwa wiki.
Akizungumza kwenye sherehe za uzinduzi huo Dar es Salaam , Waziri wa Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema serikali imebariki kusudio hilo na inashukuru kwa hatua hiyo ya Turkish Airlines.
“Hili kwa kweli tunalibariki. Mapendekezo yangu kwa Turkish Airlines ni endeleeni na tafuteni njia za kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha Afrika kama mlivyopendekeza na kwa kufanya hivyo, katika siku za karibuni, mtapata mahitaji makubwa ya kusafirisha abiria kwenda pia Mashariki ya Mbali,” alisema Dk. Kawambwa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu katika Wizara hiyo, Omar Chambo.
Dk. Kawambwa alisema hilo linatokana na kukua kwa haraka kwa mtandao wa biashara kati ya Ukanda huo wa Afrika Mashariki na Kati na Mashariki ya Mbali, hivyo kuunganisha na sehemu nyingine za Afrika.
Alisema kuanza kwa safari hizo za ndege ni mwanzo wa utekelezaji wa makubaliano ya usafiri wa anga kati ya Tanzania na Uturuki, yaliyosainiwa Januari mwaka huu.
Kwa mujibu wa Balozi wa Uturuki nchini, Dk. Sander Gurbuz, Tanzania itakuwa moja ya vituo 150 ambavyo Turkish Airlines inasafirisha abiria duniani.
Ndege ya kwanza ya Turkish Airlines yenye uwezo wa kuchukua abiria 200, ilitua JNIA hivi karibuni ikiwa na maofisa mbalimbali akiwemo Meya wa Istanbul, Kadir Topbas pamoja na wafanyabiashara mbalimbali.
Wakati wa sherehe za uzinduzi huo wa safari za ndege hiyo, watu kadhaa walishinda zawadi za tiketi za kwenda Uturuki kwa ndege hiyo akiwemo Mhariri wa Habari wa habari Leo, Mgaya Kingoba; Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Huru wa Uchumi (EPZ), Dk. Adelhem Meru na Mkuu wa Viwanja vya Ndege, Prosper Tesha.
No comments:
Post a Comment