.

.

.

.

Saturday, November 05, 2011

WARIOBA ALONGA KUHUSU DOWANS


WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema haoni nia ya dhati kwa viongozi wa ngazi za juu wa serikalini kupambana na ufisadi badala yake, suala hilo limekuwa likizungumzwa kisiasa.“Viongozi wa ngazi za juu wanazungumzia mafisadi lakini hawawachukulii hatua za kisheria, huu ni upungufu mkubwa katika utawala wetu,” alisema Jaji Warioba Dar es Salaam jana alipokuwa akizindua Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chama cha Majaji Wastaafu Tanzania (Tarja).

Warioba ambaye aliwahi kuongoza Tume ya Kero ya Rushwa wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa alisema viongozi wa Serikali wanashindwa kutofautisha masuala ya kisiasa na ya kisheria: “Sheria ni kuchukua hatua siyo kuhutubia kwenye majukwaa. Nawaasa majaji wenzangu wastaafu tujitahidi kutoa ushauri kwa viongozi na wananchi kuhusu umuhimu wa kufuata sheria,” alisema.

Kauli ya Jaji Warioba imekuja kipindi ambacho jamii ya Watanzania imegawanyika kuhusu vita dhidi ya ufisadi kutokana na watuhumiwa kutofikishwa katika vyombo vya sheria kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kukosekana kwa ushahidi dhidi ya tuhuma zinazowakabili.

Dowans walipwe
Katika hotuba yake, Jaji Warioba pia alizungumzia suala la malipo ya Kampuni ya Dowans akisema Serikali inawajibika kutekeleza amri ya Mahakama kwa kuilipa kampuni hiyo ya Costa Rica na kwamba kufanya hivyo ni kuzingatia utawala bora na wa sheria lakini akataka mafisadi waliohusika wachukuliwe hatua.

Kauli hiyo ya kwanza ya Jaji Warioba kuhusu sakata hilo la Dowans imekuja kipindi ambacho Watanzania wengi wakiwamo wanaharakati wanapinga malipo hayo ya Sh110 bilioni kwa Dowans kiasi cha kutaka kuandamana kuyapinga.

Wakati wanaharakati hao wakiwamo wanasheria kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wakipinga malipo hayo, jana Jaji Warioba alitofautiana nao akisema jambo hilo si la kisiasa bali kisheria.

Jaji Warioba aliwashangaa baadhi ya viongozi wanaosimama hadharani na kupinga hukumu hiyo ya Mahakama.

Ingawa hakuwataja kwa majina, lakini viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakipinga malipo hayo kwa nguvu zote ni pamoja na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Samwel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

“Nashangaa viongozi wa nchi inayofuata utawala bora na wa sheria wanapinga hukumu iliyotolewa na Mahakama isitekelezwe, tunaonyesha mfano gani kwa jamii tunayoiongoza? Leo tunaikataa hukumu ya kesi ya Dowans, kesho haijulikani tutaikataa kesi gani, hii itatufanya tuwe na jamii ya watu wasiofuata sheria.”

Warioba ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alitoa mfano mwingine wa kesi ya uhaini katika utawala wa Awamu ya Kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere akisema katika kesi hiyo, wananchi walilalamikia adhabu iliyotolewa na Mahakama kuwa ilikuwa ndogo mno.

“Hata Serikali ilikiri kuwa kweli adhabu hiyo iliyotolewa kwa wahaini ilikuwa ndogo, lakini haikuchukua hatua ya kuikataa adhabu hiyo, iliheshimu uamuzi wa Mahakama,” alisema Warioba.

1 comment:

  1. Enzi za uongozi wa Mwalimu Nyerere, watuhumiwa wa ufisadi wangekuwa kizuizini, kwa mujibu wa kile kilichojulikana kama uhujumu uchumi. Rais wa Tanzania ana uwezo kisheria wa kuwaweka watu kizuizini. Leo watu wanakwapua mamilioni, lakinii hawaguswi. Hii hoja ya kwamba tunangojea ushahidi wa kutosha ingawa ni kweli, yamesababisha mafisadi waendelee kuchota na kukamua bila hofu. Sasa hapo ni wazi inabidi kuchagua kati ya maovu mawili: kuwaweka watu wachache kizuizini au kuacha nchi iendelee kuteketezwa.

    ReplyDelete