WABUNGE wa CCM jana waliongoza mashambulizi dhidi ya Serikali na kufanikisha kuondolewa kwa hoja mbili zilizowasilishwa na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema.Hoja ya kwanza ya Serikali iliwasilishwa asubuhi na Waziri Mkulo ambaye alitaka Bunge liidhinishe punguzo la ushuru wa maji ya kunywa kutoka Sh69 kwa chupa hadi Sh12.
Jana jioni, Jaji Werema aliwasilisha hoja ya mabadiliko ya Sheria Mbalimbali ikiwamo ya Bodi ya Mikopo. Hoja hizo zote ziligonga ukuta na kuondolewa bungeni hadi mkutano ujao.
Mkulo
Akiwasilisha azimio hilo, Mkulo alisema kutokana na ongezeko la ushuru, maji ya chupa yamepanda kwa kiwango kikubwa, hivyo kuwafanya watumiaji wengi ambao ni wananchi wa kawaida kushindwa kumudu bei na kutumia maji ambayo siyo salama na kuhatarisha maisha yao.
“Ushuru wa bidhaa uliotarajiwa kukusanywa kwa kipindi cha Julai hadi Juni, 2012 kwa kiwango cha Sh69 kwa lita ni Sh15,549.3 milioni. Mapendekezo mapya ya kupunguza ushuru yatakusanya Sh2,704.2 milioni,” alifafanua Mkulo.
Alisema punguzo hilo litasababisha nakisi ya Sh12,845.1 milioni na kwamba, kuanzia Julai hadi Desemba, mwaka jana tayari wamekusanya Sh6,730 milioni.
“Hivyo, kwa kutumia kiwango kipya cha Sh12 kwa lita, nakisi ya mapato itapungua kutoka Sh8,819.3 milioni hadi Sh7,719.3 milioni,” alisema.
Waziri Mkulo alipendekeza maeneo ya kuziba nakisi hiyo kuwa ni kupunguza posho, fedha zinazotumika kwenye makongamano, ununuzi wa magari, gharama za uendeshaji, ununuzi wa samani, mafunzo ya ndani na nje, safari za ndani na nje na ukarabati wa majengo.
Serikali hivi sasa inatumia Sh360 bilioni kwa ajili ya posho, kati ya fedha hizo, Sh14 bilioni zinahusu wabunge.
Mpango wa miaka mitano wa Serikali unaonyesha kupunguza posho na kutafuta njia bora za kulipana mishahara mizuri.
No comments:
Post a Comment