MGOMO wa Madaktari umeshika kasi kiasi cha kusababisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kufuta ziara yake ya siku kumi iliyokuwa ikitarajiwa kuanza mkoani Mwanza leo, huku huduma za afya katika baadhi ya hosipitali nchini zikiathirika kwa kiasi kikubwa.
Ziara hiyo ambayo ilipaswa kuanza leo Machi 9, mehairishwa hadi hapo itakapopangwa baadaye huku taarifa za ndani zikieleza kuwa kuhairishwa huko kunatokana na Waziri Mkuu huyo kuwa katika majukumu ya kushughulikia kutatua mgomo wa madaktari ambao ulianza juzi. Mgomo wa madaktari umeshika kasi na kuathiri huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa (MOI) ambayo jana ilitangaza kusitishwa kwa huduma za klinini kwa wagonjwa wa nje (OPD).
Msemaji wa Taaisi hiyo, Juma Almasi alisema jana kwamba hatua hiyo imelenga kuwawezesha madaktari wachache waliopo kuhudumia wagonjwa 237 waliolazwa wodini.
“Taasisi ina wagonjwa 237 waliolazwa wodini na madaktari wanaoendela kufanya kazi ni wakuu wa idara na wenye nafasi za uongozi ambao idadi yao haizidi 15”alisema Almas.
Alifafanua kuwa katika siku za kawaida huduma za Kliniki kwa wagonjwa wa nje hutolewa na zaidi ya Madaktari 20 huku idadi ya wagonjwa ikitofautiana kutokanana na aina ya kliniki zilizopangwa kwa siku husika.
“MOI inamadaktari zaidi ya 70 na kila siku huduma za Kliniki za nje hutolewa na Madaktari zadi ya 20,kutokana na mgomo huu tumeamua kusitisha huduma za wagonjwa nje wanaokuja kwa ajili ya Kiliniki na kwamba tutaendelea kuwahudumia walioko wodini”.
Pia msemaji huyo alisema huduma nyingine zitakazopatikana katika Taasisi hiyo ni katika kitengo cha dharura.
Wagonjwa walalama
Wagonjwa wote waliofika MOI jana kupata huduma za vipimo mbalimbali katika Kliniki waliamriwa kurejea nyumbani kwao hadi watakapopata taarifa za kumalizika kwa mgomo huo kupitia vyombo vya habari.
Wakizungumza na Mwananchi baadhi ya wagonjwa na wauguzi waliitupia lawama serikali kwa kushindwa kutatua tatizo hilo ambalo walidai dalili zake zilionekana tangu mwanzo.
Mmoja wa wagonjwa hao, Kulwa Amiri (30) Mkazi wa Dar es Salaa alimtaka Rais Jakaya Kikwete,Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Mawaziri wanaokataliwa na madaktari kutafakari na kuchukua hatua zaidi ili kunusuru maisha ya wagonjwa.
“Katika mgomo wanaoathirika ni wengi siyo tu mgonjwa,wapo waangalizi wa wagonjwa nao wanapoteza muda kwa kumsindikiza mgonjwa,nauli na pia hata kazi wanazozifanya zinasimama”alisema Amiri na kuhoji:
“Hivi ni kweli serikali haioni mateso tunayopata?,inashindwa nini kuwawajibishwa hao mawaziri hao, hata kutaka kututoa sisi kafara?mbona Mh Edward Lowasa alipokuwa waziri Mkuu alijiuzulu, tunaomba watafakari kwa makini kwani tunaoteseka ni sisi”alisema Amiri ambaye alivunjika uti wa mgongo.
Wakati mgonjwa huyo akilalamikia kitendo hicho,baadhi ya ndugu wa wagonjwa wengine waliokuwa wamelazwa Wodini walifika hosptalini hapo na kuanza kuahamisha wagionjwa wao.
Marwa Chacha na ndugu zake walimhamisha, Edina Kimeta aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Mwaisela huku akieleza kufikia uamuzi huo kuwa imetokana na hali ya kutisha na isiyotabirika iliyopo katika eneo hilo.
No comments:
Post a Comment