Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
--
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete yuko njiani kwenda Washington, Marekani kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi Tajiri Zaidi na Zenye Viwanda (Group of Eight – G-8) kwa mwaliko wa Rais wa Marekani Mheshimiwa Barack Hussein Obama.
Rais Kikwete na ujumbe wake waliondoka nchini usiku wa jana,Jumanne, Mei 15, 2012 kwenda Marekani kupitia Nairobi, Kenya na London, Uingereza.
Rais Kikwete ni mmoja wa Marais wanne wa Afrika ambao Rais Obama amewaalika kuhudhuria Mkutano wa G-8 ambao unafanyika Jumamosi kwenye eneo la mapumziko ya marais wa Marekani, Camp David, katika Jimbo la Maryland.
Hata hivyo, shughuli za kikao hicho zinaanza rasmi kesho wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bibi Hillary Clinton atakapokutana na viongozi wa nchi wataohudhuria mkutano wa mwaka huu wa G-8.
Mbali na Rais Kikwete, marais wengine wa Afrika walioalikwa na Rais Obama kuhudhuria mkutano huo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mheshimiwa Thomas Boni Yayi, Rais wa Ghana Mheshimiwa Atta John Mills na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mheshimiwa Meles Zenawi.
Rais Kikwete amealikwa kushiriki katika mkutano wa mwaka huu wa G-8 ili kutoa uzoefu wake katika mapambano ya kuendeleza kilimo na kuleta usalama wa chakula katika Tanzania na Afrika kwenye kikao ambacho kitazungumzia “Hali ya Kilimo Duniani na Usalama wa Chakula” ambacho Rais Obama atakuwa mwenyekiti wake na ambacho Rais Kikwete atazungumza kwa dakika 10.
Rais Kikwete amealikwa kwa sababu ya uongozi wake katika masuala ya maendeleo ya kilimo ambao ameuonyesha kwenye uanzishwaji wa program mbali mbali hapa nchini na katika Afrika zikiwamo za ASDP (Agricultural Sector Development Programme), Kilimo Kwanza na SAGCOT (Ukanda wa Maendeleo ya Kilimo Kusini mwa Tanzania).
Rais Kikwete pia ni miongoni mwa viongozi wa Afrika walioko mbele katika kuendeleza programu ya kilimo ya Grow Africa Partnership ambako nchi saba za Afrika zinashirikiana na wadau wa kimataifa kuendeleza kilimo katika Afrika.
Mkutano huo wa G-8 unafanyika wakati kuna habari za uwezekano wa kutokea kwa upungufu wa chakula na hata kuzuka kwa baa la njaa katika baadhi ya nchi za Afrika.
Wakati wa ziara hiyo ya siku tano, Rais Kikwete pia atakutana na kufanya mazungumzo na maofisa wa Shirika la Millenium Challenge Corporation (MCC), wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel Yohanes.
Tanzania ni miongoni mwa washirika wakuu wa MCC, ambacho ni chombo cha jitihada za maendeleo cha Serikali ya Marekani na ambacho kwa sasa kinatekeleza miradi mbali mbali ya miundombinu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 698 katika Tanzania.
Katika Marekani, Tanzania inaelezwa kama nchi mfano wa mafanikio katika utekelezaji wa miradi ya MCC na Rais Kikwete anasifiwa kwa utekelezaji wa miradi hiyo unaongozwa na uwazi na ufanisi wa kiwango cha juu.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
16 Mei, 2012
No comments:
Post a Comment