.

.

.

.

Wednesday, August 14, 2013

MH. MWAKYEMBE AJITOA MHANGA NA MADAWA YA KULEVYA

WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe amesema anajitoa mhanga kuhakikisha Wizara yake inawatia mbaroni watu wanaojihusisha na usafirishaji wa dawa za kulevya kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).
“Nitajitoa mhanga juu ya biashara hiyo na siogopi vitisho vya watu, maana mimi nilishakufa siku nyingi, hatuwezi kuidhalilisha nchi yetu kiasi hicho,” alisema.
Alisema hayo juzi, wakati akieleza mkakati wa Wizara yake kudhibiti wanaosafirisha dawa hizo kupitia uwanja huo uliopewa heshima ya kuitwa jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika jijini hapa juzi.
“Dawa za kulevya sasa zinasafirishwa kupitia kiwanja cha ndege, ambacho kimepewa jina la mtu muhimu katika nchi yetu, Mwalimu Nyerere, ni aibu kwa nchi yetu na Taifa letu, kuona uwanja huo unatumika kwa biashara hiyo, nipeni muda, mimi ndiye Waziri wa Uchukuzi, hatutakubali hali hii,” alisema na kuongeza: “Pale uwanjani kuna ofisi nne, Polisi, Uhamiaji, Usalama wa Taifa na watu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege, wote nimewaagiza wanipe taarifa, walikuwa wanafanya nini hadi dawa hizo zinapita uwanjani hapo?”
Alisema anawapa notisi watu wote wanaosafirisha dawa za kulevya kupitia uwanjani hapo, watambue kuwa alishajitoa mhanga kupambana na dawa za kulevya, maana ni biashara inayodhalilisha Taifa.
Mwakyembe alipata kuugua kiasi cha kukatisha tamaa ambapo ilikuja kubainika kuwa aliwekewa sumu iliyosababisha mwili wake kuharibika na nywele kunyonyoka huku kucha zikibadilika rangi, lakini alipona alipopelekwa kwa matibabu zaidi India.
Alivitaka viwanja vyote vya ndege nchini, kuhakikisha vinaweka mikakati ya kisayansi kubaini watu wanaosafirisha dawa hizo kupitia kwenye mipaka yao.
“Na kwa hili, niviagize viwanja vyote vya ndege nchini vihakikishe kuwa vinadhibiti wasafirishaji wa dawa za kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Dola vilivyo katika viwanja hivyo,” aliongeza.
Alitaka viongozi wa dini washiriki kujenga amani nchini huku akionya vijana dhidi ya kushabikia vitendo vinavyoweza kuipeleka nchi katika migogoro ya kivita na wajifunze mifano kwa baadhi ya nchi zilizoingia kwenye vita.
Alisema uzoefu unaonesha, kuwa nchi zilizoingia katika migogoro ya kivita imekuwa vigumu kurudia hali ya kawaida na zimeendeleza vita vya wenyewe kwa wenyewe.
“Afrika Kusini, Congo DRC ni nchi ambazo zimejaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za madini, lakini kutokana na kukosa amani kwa muda mrefu, imekuwa vigumu rasilimali kufikia wananchi wote,” alisema.
Alitaka vijana kubadili tabia na mtazamo kwa kuwa ndiyo njia pekee ya kujikomboa kiuchumi na kifikra na kuacha kutumiwa na wanasiasa.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba ambaye alikuwa Mwezeshaji Mkuu katika tamasha hilo, alitaka viongozi wa madhehebu ya dini nchini waendelee kujenga amani iliyopo kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Mimi huwa naamini kuwa amani hujengwa, haiombewi, hivyo naomba viongozi wa dini mshiriki kuijenga amani nchini, kwa manufaa yetu sote,” alisema na kutaka vijana waache kulalamika bila kufanya kazi.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali la Jitambue Foundation, Isaac Mwanahapa, alisema kuwa Jitambue iliandaa tamasha hilo la vijana kwa lengo la kuwaleta pamoja ili kujadili mambo ya msingi ya Taifa.
Alisema kwa maadhimisho hayo, shirika lake liliadhimisha siku hiyo kwa kuchagua kaulimbiu ya “Tetea Amani, Okoa Kizazi Kijacho”, kutokana na nchi kugubikwa na matukio ya uvunjifu wa amani, yakiwamo ya watu kupigwa mabomu na kumwagiwa tindikali, kwenye maeneo ya ibada na hata kwenye mikutano ya kisiasa.

No comments:

Post a Comment