.

.

.

.

Wednesday, March 12, 2014

BUNGE MAALUMU LA KATIBA .............Bunge Maalumu la Katiba liliahirishwa jana asubuhi baada ya kupitisha Kanuni zitakazotumika wakati litakapoanza awamu ya pili kwa kumchagua mwenyekiti wa kudumu na baadaye kujadili Rasimu ya Katiba kabla ya kuandika Katiba Mpya itakayopelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kupigiwa Kura ya Maoni. Bunge hilo litakutana leo jioni kumchagua mwenyekiti na makamu wake watakaoliongoza kwa muda uliowekwa kisheria.
Ni masikitiko makubwa kwamba Bunge lilipitisha Kanuni hizo jana katika mazingira yasiyoeleweka, kutokana na kujirudia kwa vurugu, matusi na kejeli kati ya baadhi ya wajumbe wanaotokana na chama tawala na wa vyama vya upinzani. Chanzo cha mvurugano huo, ambao wiki iliyopita ulikuwa kidogo usababishe kurushwa ngumi bungeni ni mfumo wa upigaji kura katika kupitisha ibara za Rasimu ya Kanuni, ambao juzi na jana uliendelea kuwagawa wajumbe na kuufanya Ukumbi wa Bunge kuwa kama eneo la vilabu vya pombe.
Jambo lililo dhahiri ni kwamba Bunge hilo liliendelea kukwamishwa na siasa za vyama, ambapo wanasiasa ndani ya Bunge wanauona mchakato mzima wa Katiba kama vita ya vyama. Ni vita hiyo iliyoikwamisha Kamati ya Kanuni, ambayo ilishindwa kuhimili shinikizo la wanasiasa na mara kwa mara ililazimika kubadili uamuzi wake katika vifungu kadhaa vya Rasimu ya Kanuni. Kwa mfano, awali Kamati hiyo ilipendekeza, pamoja na mambo mengine upitishwaji wa vifungu vya Kanuni hizo ufanywe kwa kura ya siri, jambo lililokataliwa na wajumbe wa CCM ambao wanataka kura ya wazi.
Huo ndiyo msimamo wa chama hicho uliotokana na vikao mbalimbali, ambapo chama hicho kinaona hatari ya kupitishwa kwa Serikali Tatu na hatimaye kung’olewa madarakani iwapo itapigwa kura ya siri. Tunaambiwa kinaogopa usaliti wa ndani katika Kanuni ya 37 na 38, kwani kimetambua kwamba kuna baadhi ya wajumbe wake ambao wanataka kura ya siri ili wasisakamwe pale watakapopiga kura kinyume na msimamo wa chama chao. Makundi mengine, wakiwamo wajumbe kutoka vyama vya upinzani pia wanataka ipigwe kura ya siri.
Hapo hakika ndipo penye tatizo na ndiyo hasa chanzo cha shughuli za Bunge kuchelewa kwa zaidi ya wiki moja, hivyo kuvuruga ratiba nzima ya Bunge hilo. Inasemekana shinikizo la CCM limeilazimisha Kamati ya Kanuni ipendekeze kwamba Kanuni ya 37 na 38 zieleze tu kwamba utaratibu wa uamuzi utakuwa ni wa kura, bila kusema ni ya siri au ya wazi. Kinachoshangaza ni kwamba wajumbe wa Kamati ya Mashauriano walioteuliwa na mwenyekiti kupata mwafaka wa masuala mbalimbali, wakiwamo wajumbe wa CCM walikubaliana kwamba kura iwe ya siri, lakini walishangaa kuona CCM kikiwageuka na kuishinikiza Kamati ya Kanuni ipendekeze kama tulivyobainisha hapo juu.
Sisi tunasema hali hiyo ya kuendesha mchakato wa Katiba pasipo kuwapo maridhiano ndani ya Bunge kutazaa Katiba ya mpito badala ya Katiba ya kudumu. Maana yake ni kwamba haitazingatia masilahi mapana ya wananchi na badala yake itakuwa na upungufu usiovumilika wa kulinda matakwa ya watu wachache, hivyo kulazimika kufanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara. Ndiyo maana tangu mwanzo wajumbe wamekuwa wakikubaliana kutokubaliana. Uchaguzi wa Mwenyekiti wa kudumu leo jioni ufanywe kwa umakini mkubwa, vinginevyo Bunge litasambaratika kabla ya kumaliza kazi yake

No comments:

Post a Comment