.

.

.

.

Tuesday, September 16, 2008

SAKATA LA MAUAJI AFRIKA KUSINI

Zanzibar yaulaumu ubalozi wa Tanzania Afrika Kusini

Na Mwandisho Maalum
Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini umelaumiwa kwa kupuuza taarifa za vifo vya
Watanzania 12 wanaodaiwa kuuawa katika mazingira ya kutatanisha nchini humo wiki
mbili zilizopita.
Wazazi wa vijana wawili waliouawa katika matukio yanayosadikiwa kuwa yanatokana na chuki dhidi ya wageni, Mzee Mussa Makungu, 26, na Rajab Suleiman Mrisho, 24, wameutupia lawama ubalozi huo wakidai kuwa haujali maisha ya Watanzania kwani unaonekana haufanyi kazi zake za kibalozi zaidi ya kutumia fedha za walipa kodi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Suleiman Mrisho, baba wa marehemu Rajab, alisema ni vyema ubalozi huo ukawa karibu na raia wa Tanzania wanaoishi nchini humo kwani iliwachukua muda wa siku nne tangu wapewe taarifa za kuuawa raia hao kabla ya kuanza kufuatilia.
Alisema walipokea taarifa za vifo kutoka kwa rafiki wa marehemu kwamba vijana wao
wameuawa wakati wakiwa nyumbani kwao jijini Port Elizabeth.
Baba wa marehemu huyo alisema mtoto wake alikuwa akifanya kazi katika kampuni moja
ya mafuta katika kipindi chote tangu alipowasili Afrika ya Kusini mwaka 2003.
Abdallah Othman Ali, mjomba wa marehemu wa Mzee Mussa Makungu, alishangazwa na taarifa za Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania inayodai kuwa vijana hao walikuwa wakijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na kwamba waliuawa katika ugomvi baina ya Watanzania wenyewe.
Wananchi wengi wa visiwani hapa wameitaka Wizara ya Mambo ya Nje kuacha kutoa
matamshi bila ya utafiti na badala yake ifanye uchunguzi wa kina kujua sababu za kuuawa kwa raia wao wa Tanzania.
Walisema kuwa imekuwa ni kawaida kwa wizara hiyo kutoa majibu ya mkato yasiyo na uchunguzi wowote wakati kunapotokea matukio kama hayo.
Alitoa mfano wa kijana Suleiman Abdallah Salim, aliyekamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na ugaidi na kukaa jela kwa miaka kadhaa kabla ya kutolewa akiwa ameathirika kiafya, lakini serikali haijashughlikia suala lake.
Mapema mwaka huu, vikundi vya vijana wa Afrika Kusini vilianzisha mashambulizi dhidi ya raia wa kigeni wanaofanya kazi nchini humo, hasa kutoka nchi jirani ya Msumbiji, wakidai kuwa wanapora ajira zao. Hakuna Mtanzania aliyeripotiwa kudhurika na vurugu hizo.
Lakini kumekuwa na habari kuwa Watanzania 12 wameuawa katika mashambulizi hayo, habari zilizotiwa nguvu na kuwasili kwa maiti za vijana hao wawili waliouawa kwa kupigwa risasi.
Katika zaira yake nchini Tanzania, kiongozi wa chama tawala cha Afrika Kusini cha ANC, Jacob Zuma aliwaomba radhi watanzania kwa vitendo hivyo vya chuki dhidi ya wageni na kueleza kuwa chama chake hakipo pamoja na makundi ya vijana hao wanaowashambulia wageni.

No comments:

Post a Comment