.

.

.

.

Friday, October 31, 2008

UKWELI AU USANII WA SELIKALI KUJULIKANA LEO


Mwanasiasa mkongwe nchini na Naibu Gavana wa zamani wa BoT, Bob Nyanga Makani, amesema kuwa leo ndio ukweli au usanii wa serikali utajulikana. Makani, ambaye pia aliwahi kuwa naibu mwanasheria mkuu wa serikali katika awamu ya kwanza, alisema alishangaa, anashangaa na atashangaa zaidi iwapo tuhuma hizo za wizi wa fedha za EPA zitazidi kufanywa kuwa madai badala ya jinai.
Makani, ambaye ni mtu aliyewahi pia kushika nyadhifa mbalimbali za ujumbe na uenyekiti wa bodi mbalimbali za mashirika na taasisi za umma, alisema kilichofanyika BoT ni jinai na kwamba matumaini ya Watanzania ni kuona watu wanakamatwa.
"Si tuhuma za madai zile, ni makosa ya jinai, watu wameiba fedha huwezi kuwafanyia kesi ya madai," alisema Makani na kuongeza:
"Lakini siku si zimekwisha! Kuna kitu gani... hebu tumsubiri Kikwete tuone atafanya nini kama alivyosema mwenyewe, tusimhukumu kabla."
Duru za kiserikali zinasema baadhi ya akaunti za vigogo wa makampuni yaliyochota mabilioni hayo kwa mgongo wa wafanyakazi wadogo, zimeweza kuchunguzwa na fedha kuchukuliwa.
Taarifa hizo zinasema kukamatwa kwa akaunti za vigogo hao kunatokana na kuangalia mzunguuko mzima wa fedha kutoka malipo yaliyofanywa BoT hadi zilizoishia.
"Hawa watu walitumia wafanyakazi wao kusaini fedha, lakini uchunguzi uliona mwisho wa fedha ziliingia katika mikono ya vigogo kwa kuingia katika akaunti zao," kilidokeza chanzo huru kutoka duru za kiserikali."
Kwa mujibu wa duru hizo, iwapo rais ataamua kutumia mamlaka yake kufikisha wote waliohusika mahakamani, basi kuna vigogo ambao ni wafanyabiashara wakubwa, mawakili maarufu na baadhi ya maafisa wa serikali, watakumbwa na zahama hiyo.
Ufisadi wa EPA ulibainika katika hesabu za BoT za mwaka 2005/06, baada ya ukaguzi uliofanywa na kampuni ya Ernst& Young, ambayo ilipewa kazi iliyoachwa kiporo na Deloitte&Touche ya Afrika Kusini iliyositishwa ghafla kuendelea na ukaguzi huo.
Kampuni hiyo ya Afrika Kusini ilisitishwa baada ya kubaini ufisadi wa Sh40 bilioni zilizochotwa na Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited.
Baada ya Deloitte &Touche kuzuiwa kuendelea na kazi, mwaka jana serikali mwaka jana ilimwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kutafuta kampuni ya kimataifa, kufanya ukaguzi huo kubaini ukweli.
Ofisi ya CAG iliteua kampuni hiyo ya kimataifa ya Ernst&Young, ambayo ilibaini ufisadi wa fedha hizo zaidi ya sh 133 bilioni, ambazo zilichotwa na makampuni 22.
Makampuni 13 yalijichotea sh 90.3 bilioni, ni pamoja na Bencon International LTD of Tanzania, Vb & Associates LTD of Tanzania, Bina Resorts LTD of Tanzania, Venus Hotel LTD of Tanzania, Njake Hotel &Tours LTD, Maltan Mining LTD of Tanzania.
Mengine ni Money Planners & Consultants, Bora Hotels & Apartment LTD, B.V Holdings LTD, Ndovu Soaps LTD, Navy Cut Tobacco (T) LTD, Changanyikeni Residential Complex LTD na Kagoda Agriculture LTD.
Kwa upande wa makampuni tisa yaliyochota Sh42.6 bilioni ni pamoja na G&T International LTD, Excellent Services LTD, Mibale Farm, Liquidity Service LTD, Clayton Marketing LTD, M/S Rashtas (T) LTD, Malegesi Law Chambers (Advocates), Kiloma and Brothers na KARNEL LtD.
Makampuni mengine mawili ambayo ni Rashtas (T) na G&T International LTD, kumbukumbu zake ikiwemo nyaraka za usajili katika daftari la Msajili wa Majina ya Makampuni na Biashara (BRELA), hazikuweza kupatikana.
Kufikia mwaka 1999 deni katika EPA lilifikia dola 623 milioni, ambazo kati ya hizo dola 325 milioni zilikuwa ni deni la msingi na dola 298 ni riba na kisha baadaye deni likaongezeka hadi kufikia dola 677 milioni.
Hata hivyo, chini ya Mpango wa Kununua Madeni (Debt Buy Back Scheme) wa mwaka 1994 kati ya serikali na Benki ya Dunia (WB), waliokuwa wanaidai BoT waliombwa wakubali kulipwa sehemu tu ya fedha wanazodai, wapo waliokubali na wengine kukataa na kuongeza hadi mwaka 2004 taarifa zinaonyesha jumla ya dola 228 zililipwa chini ya mpango huo.
EPA ni akaunti ya madeni ambayo ilitumika wakati wa Mfumo wa Ujamaa, ambayo akaunti yake ilikuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) chini ya usimamizi wa BoT.
Mwaka 1985, EPA ilihamishiwa moja kwa moja BoT na ndipo mwaka juzi kulipoibuka utata wa tuhuma za ufisadi katika akaunti hiyo kwa mahesabu ya mwaka 2005/06, ambayo utata huo ulisababisha Ernst&Young kufanya ukaguzi kuanzia Septemba sita na kukabidhi ripoti yake kwa CAG mapema Desemba mwaka jana

No comments:

Post a Comment