.

.

.

.

Tuesday, September 13, 2011

SIMULIZI YA KUSIKITISHA JUU YA AJALI YA MELI ZANZIBAR


Baharia Rashid Said Rashid wa meli ya MV Spice Islander, iliyozama na kuua takribani watu 240 huku wengine 619 wakinusurika visiwani Zanzibar juzi, amesema waligawa maboya ya kujiokoa kwa abiria na kuwavalisha watoto kisha kuwaondoa melini kupitia madirishani kabla ya kuzama.Akizungumza na gazeti NIPASHE akiwa amelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, jana, alisema kabla ya meli hiyo iliyokuwa na mabaharia 12 kuzama majira ya saa 7:00 usiku wa Ijumaa iliyopita eneo la Nungwi, waliomba msaada kwa meli nyingine iliyokuwa inapita lakini hawakufanikiwa.Said ambaye ni mkazi wa Shangani, alisema baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kabla ya meli kupinduka, abiria walimtaka nahodha atoe taarifa kwao kama meli inazama na alifanya hivyo, “Tulijaribu kufanya kila jitihada ili kuokoa hali hiyo, lakini tulishindwa na tukaamua tuiache meli na kuanza kutoka, hapo tena kila mmoja alikwenda kwa upande wake,” alisema.Hata hivyo, alisema hafahamu kama mabaharia wenzake na nahodha wapo salama au wamekufa kwa sababu mara ya mwisho aliwaona kabla ya chombo kupinduka na kuzama, “Kwa kweli siwezi kusema kama ni uzembe au la umefanyika, lakini wakati inatokea hali hii tulipishana na meli ya MV Jitihada na kuwapa ishara ya kuzama, lakini hawakutusaidia,” alisema baharia huyo.Alisimulia kuwa walichukua jitihada mbalimbali za kuwapa ishara, lakini hawakufanikiwa na hawezi kusema kama walidharau au hawakuwaelewa walichokuwa wakikitafuta kutoka kwao. [hiyo ni nukuu ya NIPASHE]

Katika mazungumzo yake na MTANZANIA katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, ZanzĂ­bar jana baharia huyo alisema abiria wengi walikufa kutokana na uzembe.Baharia huyo aliyelazwa hospitalini hapo, alisema iwapo kama waokoaji wangewasili mapema eneo la tukio baada ya kupata taarifa, abiria wengi wangeokolewa kwa kuwa ulikuwa na sababu za kuwaokoa, ”Ajali ni ajali, lakini kwa hii ya kwetu nasema wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya uzembe wa wahusika... “Lakini, hayo tuyaache kwa sababu yameshatokea, nakumbuka wakati tunatoka Dar es Salaam tumbo lilikuwa likiniuma, kwa hiyo, muda mwingi nilikuwa nimelala chumbani kwetu... Ilipotimia kama saa 7.00 usiku, Bubu mmoja ambaye ni mfanyakazi wenzetu alikuja chumbani kwetu na kutuonyesha kwa ishara, kwamba tutoke nje hali imeharibika, tukamuuliza kuna nini akazidi kutwambia tokeni nje, tulipoona anazidi kutusisitizia tukatoka nje... Nilipofika nje tu, nikakuta maji yameanza kujaa melini, mimi na wenzangu tukaanza kuyatoa kwa ndoo na mashine za pampu.“Baadaye umeme ukazimika na mashine zikashindwa kufanya kazi. Sasa tukaendelea kuyatoa kwa ndoo, lakini hatukuweza lolote kwa sababu yalikuwa yakiingia kwa kasi sana... Tulipoona hivyo tukaambizana kwamba hali ni mbaya, nikawaambia wenzagu tumwambie kapteni (nahodha) awatangazie abiria. Tulipomwambia kapteni akakubali akatangaza kwamba hali ni mbaya kwa hiyo, abiria wote wawe waangalifu wakati taratibu nyingine zikifuatwa,” alisema Rashid. Kwa mujibu wa baharia Rashid, baada ya tangazo hilo, abiria walihamaki na kuanza kukimbia ovyo kuokoa maisha yao huku wakipiga kelele za kuomba msaada. “Tangazo hilo liliwatisha abiria na wakati huo maji yalikuwa yakizidi kuingia ndani, nilipoona hivyo, nikachukua ‘my life jacket’ (makoti ya kuogelea) nikawa nawavisha abiria mmoja baada ya mwingine na kumtupa majini... Nilifanya kazi hiyo kwa muda kidogo, baadaye nilipoona maji yamezidi nikaamua kujitosa baharini baada ya kuvaa life jacket... Nilipojitosa majini, kuna abiria walikuwa wakijirusha majini na kuniangukia, kwa hiyo, nikaamua kulivua lile life jacket ili niwe huru kuongelea na kuwaokoa wengine... Nilipokuwa majini nilishtuka kuona watu wamezagaa majini na wengine wamekufa, kwa hiyo, nilichokuwa nikifanya nilikuwa nikizivua life jacket zilizokuwa katika maiti na kuwavalisha wengine ambao nilikuwa nikiwaweka katika turubai moja ambalo ni maalumu kwa ajili ya uokoaji.“Wakati nikiwa katika turubai hilo, kuna abiria walikuwa jirani kabisa na mahali ilipokuwa meli, nikawaambia ondokeni hapo, meli itawapindukia, wakabisha na mwishowe kweli iliwafunika kwa sababu wakati nawaambia nilikuwa nikiiona imeshaanza kuegemea upande mmoja,” alisema Rashid na kulengwa na machozi na kuongeza, “Nilipoona wenzangu wamefunikwa, niliumia sana lakini nikasema hiyo ni mipango ya Mungu. Baada ya hatua hiyo nikamuona mzee mmoja akiwa na mtoto wake amembeba mgongoni, akaniomba, akasema mwanangu naomba umuokoe mwanangu, nikakubali, nikamwambia mzee tulia... Nikamchukua yule mtoto nikampeleka katika lile turubai nilikokuwa nimewaweka wengine.

“Nilipomuokoa huyo mtoto, mbele yangu nikaona watu watatu wanalalamika, pembeni kulikuwa na mwanamke mmoja akilia kwa huruma... Nikamfuata huyo mwanamke, nikamkuta na kitu kama mkeka hivi amekishika, nikamwambia achia huo mkeka, akakataa akasema nitakufa, nikamzaba kibao usoni kwa nguvu, akaachia ule mkeka, nikamkamata na kumpeleka kwenye lile turubai... Baadaye nguvu zilianza kuniishia, nikawa nashuhudia kabisa wenzagu waliokuwa pembeni na sisi wakiwa wanapoteza maisha mmoja baada ya mwingine, yaani niliumia sana na nadhani hili tukio litachukua miaka mingi sana kunitoka kichwani.“Katika lile turubai nilikuwa na abiria kama 15 niliokuwa nimewaokoa, baadaye nikaona wanaanza kuchoka kwa njaa, nikaamua kujitosa tena majini nikaanza kukusanya juice za Azam zilizokuwa zimetapakaa majini... “Nilipopata za kutosha nikaanza kuwanywesha wale abiria wapate nguvu na kila aliyekuwa akinywa fumba moja namkataza namnywesha mwingine,” alisema.Pamoja na hatari ya kifo aliyokuwa akiiona mbele yake, baharia huyo alisema alikuwa akiwapa moyo wenzake kwa kuwaambia kuwa mahali walipokuwa palikuwa salama na hakukuwa sababu ya kuhofia maisha yao.“Nilikuwa nawapa matumaini nikawa nawaambia tutapona tu hata kama tutapeperushwa na upepo hadi Tanga au Mombasa, lazima tutaokolewa. Ilipotimia kama saa 12.00 alfajiri, niliona helkopta kwa mbali, nikamwambia mfanyakazi mwenzagu anaitwa Almada, achukue taa moja hivi, akaichukua akainyanyua kuwaonyeshea wale wenye helkopta waweze kutuona, lakini hawakutuona kwa sababu walikuwa mbali ingawa sisi tulikuwa tunaiona hiyo helkopta. Nilipoona hawatuoni, nikamwambia tunyooshe bendera, alipoinyoosha wakati huo helkopta ilikuwa imekaribia ndipo wakatuona na kutufuata huku meli za uokoaji kama Sea Bus na Sea Express zilizokuwa zikiongozana na hiyo helkopta zikatufuata na kutuokoa.“Lakini, nakwambia kuna uzembe umefanyika… kama waokoaji wangefika mapema watu wasingekufa kwa kiasi hiki kwa sababu baada ya meli kuanza kupoteza mwelekeo, tulipiga simu polisi na bandarini kuomba msaada, lakini hawakufika hadi saa 12.00, sasa hapa tumlaumu nani, serikali au nani? Mungu anajua,’ alisema.source: NIPASHE

No comments:

Post a Comment