HATIMAYE Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar es Salaam imewapa dhamana mawaziri wawili waandamizi katika Serikali ya Awamu ya tatu baada ya kutimiza masharti ya dhamana. Mawaziri hao Basil Mramba aliyekuwa Waziri wa Fedha na mwenzake Daniel Yona wa Nishati na Madini, waliachiwa huru saa 5:25 asubuhi hatua iliyowafanya ndugu na jamaa zao waliofurika mahakamani hapo kububujikwa machozi. Awali mawaziri hao wanatuhumiwa kuipa kampuni ya M/S Alex Stewart mkataba wa kudhibiti madini kinyume cha sheria na kulisababishia taifa hasara ya sh. bilioni 11.7, walikata rufaa Mahakama kuu kuomba kulegezwa masharti ya dhamana. Mapema leo asubuhi katika hali isiyo ya kawaida Mramba aliruka kutoka kwenye ngazi ya juu za mlango wa karandinga la Magereza alipofikishwa Kisutu hali iliyowaacha hoi waandishi waliokuwa mahakamani hapo. Waandishi wetu waliokuwa mahakamani hapo walieleza kuwa Mramba na Yona walifikishwa mahakamani hapo saa 1:45 asubuhi na kukuta jopo la waandishi na wapigapicha likisubiri kwa hamu kujua hatma ya dhamana yao baada ya 'kupiga kwata' kufuatilia tangu Ijumaa iliyopita bila mafanikio. Katika mazingira hayo, Mramba aliamua kuruka kutoka kwenye ngazi kwa lengo la kukwepa wapigapicha. Mramba ambaye tofauti na siku zilizopita ambapo amekuwa akifika mahakamani akiwa amevalia 'Kaunda suti' leo alivaa shati la drafti huku akiwa ameshikilia nyaraka mkononi kama kawaida yake. Baada ya kuingia mahakamani alianza kupitia nyaraka hizo huku mwenzake Yona aliyevalia shati la maua akiwa ametulia kimya. Wakati wakimsubiri hakimu, Mramba alizungumza na ndugu zake kwa ishara na kutoa tabasamu la kulazimisha. Kesi hiyo ambayo ilikuja kwa ajili ya uhakiki wa nyaraka ilikuwa na hati nne kwa ajili ya Mramba.
Hati mali zilizoletwa mahakamani ni namba 42578 ya Khatib Senkoro iliyopo Mikocheni yenye thamani ya sh. milioni 395. Hati ya pili ni namba 44755 kutoka kwa Haruni Mohamed ipo Chang'ombe Kiwanja namba 138 chenye thamani ya sh. bilioni 1.2 na ya tatu ni Kampuni ya Kilimanjaro Mine Limited yenye thamani ya sh. milioni 976. Hati ya nne ni nyumba ya Mramba iliyopo Kawe ina thamani ya sh. milioni 547 . Jumla ya thamani ya mali zote ni sh. bilioni 3.4
Yona aliwasilisha hati namba 97467 ya mali ya sh. milioni 443, hati namba 59935 ya thamani ya sh. bilioni 2.2 na hati ya nyumba namba 57230 iliyopo Makongo juu yenye thamani ya sh. milioni 420.3 . Yona aliwasilisha hati za mali yenye thamani ya jumla sh.bilioni 3.63. Baada ya kukamilisha taratibu hizo, Mahakama hiyo imeridhia na kuwachia huru kwa dhamana. Upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na itatajwa tena Januari 2 mwakani. Walipotoka mahakamani wananchi waliofurika walizomea kwa kuita wezi hao...!hadi magari yao yalipotoka eneo la mahakama.
No comments:
Post a Comment