KATIKA tukio lisilo la kawaida nchini, mafuvu 40 ya vichwa vya watu yamegundulika yakiwa yamefukiwa ndani ya pango lililo chini ya mti wa mbuyu, kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga.
Matukio kama hayo yamekuwa yakiripotiwa kwenye nchi zilizowahi kukumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe, lakini Jeshi la Polisi limeeleza kuwa limegundua mafuvu hayo katika kijiji cha Mayangi kilicho katika Kata ya Ukenyenge tarafa ya Negezi wilayani Kishapu.
Kamanda wa polisi mkoani Shinyanga, ACP Shaibu Ibrahim alisema jana kuwa mafuvu hayo yalikutwa pamoja na mabaki mengine ya miili ya binadamu.
Alisema tukio polisi walibaini mabaki hayo ya binadamu Januari 13 wakati walipoenda kwenye eneo hilo majira ya saa 10:35, ingawa taarifa yake haikueleza kiini cha kwenda eneo la tukio kufanya uchunguzi uliosababisha kugundulika kwa mabaki hayo.
"Kati ya mabaki hayo, mafuvu 35 yaliweza kuhesabika na matano mengine kukutwa vipande vipande na yalikutwa yamefunikwa pangoni chini ya mti wa mbuyu," alisema
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, inaonekana mafuvu na mifupa hiyo ya watu wasiofahamika, imekuwapo eneo hilo muda mrefu bila kujulikana.
"Pia hatukuweza kufahamu mifupa na mafuvu haya na ya watu wa jinsia gani lakini tumeyahifadhi kwa ajili ya uchunguzi zaidi ili kubaini umri na jinsia za watu hao," alisema.
MAfuvu hayo yamechukuliwa na kuhifadhiwa kwenye kituo cha polisi cha mkoa jana huku polisi hao wakiwa na vikao kadhaa vya ndani kujadili suala hilo.
Iwapo si mauaji ya watu wengi, mabaki hayo yanaweza kuwa yanatokana na imani za watu wengi kuwa wakoloni walipoondoka waliacha madini, na hasa rubi, chini ya miti ya mibuyu, imani ambayo hufanya watu wengi wanaoishi kwenye maeneo yenye madini kuchimba mashimo marefu karibu na mibuyu kusaka vito hivyo.
Hata hivyo, idadi ya mafuvu hayo ni kubwa. Si rahisi watu 40 kuchimba shimo moja na kuingia kusaka madini yaliyoachwa na wakoloni na ukweli kwamba mabaki hayo yalikuwa yamefunikwa unaacha maswali mengi, hasa kwenye maeneo hayo ambayo yamekuwa na mauaji makubwa kutokana na imani za kishirikiana
No comments:
Post a Comment