.

.

.

.

Wednesday, March 11, 2009

MSHITAKIWA LEMA BADO MGONJWA

Uwezekano wa mshtakiwa wa 12 katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja, Rashidi Lema, kupanda kizimbani kwa utetezi wake hivi karibuni ni mdogo kutokana na hali yake kiafya kuwa tete. Mshtakiwa huyo ambaye alishindwa kuhudhuria kesi inayomkabli na polisi wenzake, amelazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa wiki moja sasa ili apate matibabu dhidi ya maradhi yanayomsumbua.

Lema ambaye hupo chini ya uangalizi mkali wa askari Magereza ambao wamekuwa wakibadilishana zamu kila baada ya saa kadhaa, amelazwa jengo la Mwaisela wodi namba tano iliyopo ghorofa ya pili hospitalini hapo. Habari kupitia chanzo chake kilichopo wodini hapo, kilisema mshtakiwa huyo bado hali yake sio nzuri kutokana na kwamba hana nguvu na amekuwa akisaidiwa pindi anapotaka kuinuka. ``Lema bado anaumwa sana kwani akitaka kula lazima apate usaidizi wa kunyanyuliwa na hivyo habari za kusema kwamba anaendelea vizuri zinapotosha ukweli,`` kilisema chanzo hicho. Aidha chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa, mshtakiwa huyo licha ya kuhitaji msaada wa kunyanyuliwa pia usoni ametokwa na vidonda na ongea yake inaonyesha wazi kuwa bado ana maumivu makali na anahitaji msaada zaidi wa kitabibu.

Upande wa waendesha mashtaka wa serikali katika kesi hiyo ulikaririwa jana na chombo kimoja cha habari kuwa, unasubiri hali ya mshtakiwa huyo itakapotengamaa waombe mahakama imwite ili atoe utetezi wake. Katika habari hizo za jana, Uongozi wa Muhimbili ulikaririwa ukisema kuwa mgonjwa huyo anaendelea vizuri. Lema alihamishiwa hospitalini hapo akitokea hospitali ya Wilaya ya Temeke alikokuwa akitibiwa awali baada ya kuzidiwa akiwa mahabusu ya gereza la Keko.

Mshtakiwa huyo amebeba ushahidi muhimu unaosubiriwa kwa hamu na baadhi ya watu waliokuwa wakifuatilia kesi hiyo. Lema ndiye alibadili sura nzima ya kesi ya mauaji inayowakabili yeye na polisi wenzake baada ya kwenda kwa mlinzi wa amani na kueleza kwa kituo jinsi mauaji ya wafanyabiashara hao yalivyofanyika. Pamoja na Lema na washitakiwa wengine, kesi hiyo pia inamkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, Abdalah Zombe akiwa ni mshitakiwa wa kwanza. Zombe pia alikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam. Mauaji hayo yalifanyika mwaka 2006.

No comments:

Post a Comment