.
.
Monday, May 11, 2009
DARAJA KIGAMBONI KUJENGWA KARIBUNI
UJENZI wa daraja la Kigamboni, Dar es Salaam, unatarajiwa kuanza wakati wowote mwaka huu, baada ya mkandarasi kupatikana. Mbunge wa Kigamboni, Mwinchoum Msomi, alisema hayo jana alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005. Alikuwa akizungumza kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM ya Jimbo hilo katika ukumbi wa Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam. Kikao hicho kilifunguliwa na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Temeke, Ayoub Chamshama. Katika taarifa hiyo inayoanzia Oktoba, 2005 hadi Aprili, mwaka huu, Msomi alisema serikali ilishatangaza zabuni ya kumtafuta mjenzi wa daraja hilo na alitarajiwa kupatikama mwezi uliopita. Alisema ujenzi wa daraja hilo utakuwa chini ya utaratibu wa Buld- Operate- Transfer (BOT) utakaosimamiwa na Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Alisema licha ya mchakato wa ujenzi wa daraja hilo, kimenunuliwa kivuko kipya cha MV Magogoni kwa gharama ya sh. bilioni nane. Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba abiria 2,000 na magari madogo 60 kwa wakati mmoja. Msomi alisema kwa msaada wa Benki ya Dunia, vivuko vya zamani vya MV. Kigamboni na MV. Alina vitafanyiwa ukarabati mkubwa. Alisema tayari kivuko cha MV. Kigamboni kimepelekwa kufanyiwa ukarabati kwa gharama ya sh. bilioni mbili. Kuhusu ujenzi wa barabara katika kipindi hicho, Msomi alisema barabara ya Kilwa yenye urefu wa kilomita 11.5 kati ya Bendera Tatu hadi Mbagala Rangitatu, imejengwa kwa kiwango cha lami. Ujenzi wa barabara hiyo umegharimu sh. bilioni 25, ambapo serikali ya Japan, imesaidia sh. bilioni 23 huku sh. bilioni mbili zikiwa zimetolewa na serikali ya Tanzania. Katika kipindi hicho pia serikali imejenga kwa kiwango cha lami kilomita 1.4 za barabara ya Feri – Pembamnazi na barabara nyingine kadhaa zikiwa zimewekwa changarawe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment