.

.

.

.

Thursday, May 28, 2009

UGUNDUZI WA NYAYO KWENYE MIAMBA YA USAMBARA

ALAMA za nyayo za Binadamu wa kale wanaokadiriwa kuishi zaidi ya miaka milioni moja na nusu iliyopita, zimegundulika kwenye miamba ya Milima ya Usambara Magharibi.

Nyayo hizo zipo maeneo yenye kutunza Visukuku iliyoko katika eneo la Madala Kijiji cha Mambo kilichopo Kata ya Sunga Tarafa ya Mlalo wilayani Lushoto mkoani hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo alibainisha hayo juzi wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Alisema hatua hiyo ni mafanikio ya utafiti uliofanywa na Mtaalamu wa Kitanzani wa upigaji picha na utengenezaji wa filamu za kihistoria nchini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Professa Edward Mgema.

Kalembo alisema ugunduzi wa nyanyo hizo ni hatua muhimu kwa Taifa na kwamba pia itauweka mkoa wa Tanga kuwa eneo muhimu la historia za Afrika na dunia nzima kwa ujumla.

Alisema mkoa huo, umeanza kufanya maandalizi ya kutengeneza filamu ya kipekee yenye matukio yanayoambatana na ugunduzi wa nyayo za binadamu, wanyama wa kale na kuonyesha magofu ya ngome, majengo ya zama za maharamia wa kiarabu na kiajemi na wakoloni wa Kijerumani.

Alisisitiza kuwa kutokana na umuhimu huo, filamu hiyo itaonyesha watu kutoka koo mbalimbali za makabila ya Wadigo, Wasambaa, Wasegeju, Wazigua na makabila mengine kutoka bara ambao ni waathirika wakubwa wa biashara ya utumwa iliyofanywa kwa zaidi ya karne 19.

Naye Profesa Mgema alisema litachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza wawekezaji kwenye sekta ya utalii na hatimaye kuboresha maisha ya wananchi kimkoa na taifa kwa ujumla.

Kutokana na hatua hiyo Profesa Mgema alivitaka vyombo vya habari kutumia fursa hiyo muhimu kutangaza mafanikio ya utafiti huo, ili kuiweka nchi ya Tanzania katika nafasi nzuri ya historia za kidunia.

“Uzinduzi huu ni hatua kubwa sana kidunia, kusema kweli tangu nimeanza kazi hii kwa kipindi cha miezi sita hapa Tanga nimebaini mkoa huu una rasilimali kubwa kuliko mkoa mwingine wowote hapa nchini kwenye yale maeneo niliyotembelea, huu ni utajiri wa kipekee kwa mkoa huu,”alisisitiza Profesa Mgema.

Mradi wa kupiga na kutengeneza filamu za kihistoria za Taifa, unajulikana kama Fukwe za Dhahabu (The goldenshores Documentary Inc) ambao ulianzishwa Oktoba 2006.

No comments:

Post a Comment