.

.

.

.

Friday, June 19, 2009

KIKWETE AAMURU KUPUNGUZWA KWA IDADI YA WANAOSAFIRI SAFARI ZA NJE


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Jakaya Mrisho Kikwete ameamuru kupunguzwa kwa idadi ya watu katika msafara wa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika safari za nje ya nchi ili kupunguza gharama. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, aliliambia Bunge jana kuwa hatua hiyo imekuja baada ya kuonekana kuwa Sh bilioni nane zilizotengwa mwaka jana kwa kazi hiyo ya safari hazitoshi. Alisema hatua hiyo inafanya mamlaka husika kuanza kuangalia namna nzuri ya kuandaa watendaji wanaopaswa kufuatana na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Alisema utaratibu unaotumika katika kuchagua nani afuatane na viongozi wa juu wanaposafiri unazingatia vigezo mbalimbali kama vile wapambe wa viongozi, maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambao hawana budi kufuatana na viongozi kwa mujibu wa itifaki.
Alisema pia wapo viongozi wanaoteuliwa kujiunga na misafara hiyo kutokana na kusudio na madhumuni ya safari ambapo uteuzi hufanywa na ofisi za viongozi hao kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa upande wa Zanzibar na Ofisi ya Spika kwa upande wa wabunge. Alisema katika uteuzi huo, vigezo vya jinsia, uwakilishi kutoka pande zote mbili za Muungano na wa kambi ya Upinzani huzingatiwa. Alisema kila wakati viongozi wakuu wanaposafiri nje ya nchi, waandishi wa habari wamekuwa wakijumuishwa katika misafara hiyo na inapotokea kuwa viongozi wamekaribishwa kutembelea nchi jirani, basi wakuu wa mikoa inayopakana na nchi hizo huteuliwa kufuatana na viongozi. Alisema kwa kuzingatia vigezo hivyo, makundi ya viongozi yanayofuatana na viongozi wakuu wa nchi ni mawaziri wa pande zote za Muungano, wabunge na watendaji wa idara mbalimbali za Serikali kutegemeana na madhumuni ya ziara. Waziri Membe alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Zulekha Yunus Haji (CCM), aliyetaka kujua ni utaratibu gani unaotumika kuchagua viongozi wanaofuatana na Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu katika ziara nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment