.

.

.

.

Friday, June 26, 2009

OLE SENDEKA ATUPA DONGO KWA MH.MASHA

MBUNGE wa Simanjiro, Christopher Ole-Sendeka (CCM), amesema kero hazitaweza kuisha kama serikali haitashughulikia tuhuma za ufisadi dhidi ya kampuni za Kagoda na Deep Green Finance, akidai kuwa kuna waziri katika serikali ya awamu ya nne anayeikingia kifua.
Ole-Sendeka anaingia kwenye orodha ya kundi la wabunge walioamua kulishughulikia Baraza la Mawaziri kwa kulirushia tuhuma mbalimbali tangu kuanza kwa mijadala ya hotuba za makadirio ya matumizi ya wizara mbalimbali.
Bila ya kumtaja jina, Sendeka alituhumu waziri huyo kuwa mmoja wa wamiliki wa kampuni ya Deep Green, ambayo inatuhumiwa kwa ubadhirifu wa mamilioni ya fedha za walipakodi na hivyo akataka kigogo huyo abanwe ili asaidie kupatikana kwa dola 10 milioni za Kimarekani ambazo kampuni hiyo inadaiwa kuzichukua.
Ole-Sendeka alitoa kauli hiyo jana wakati akichangia makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Akionyesha dalili za kuuma na kupuliza, Sendeka alisema ana imani na serikali ya awamu ya nne, lakini akasema kuwa tuhuma hizo zisiposhughulikiwa wabunge wa CCM wataendelea kuisakama serikali.
“Tunajua kiporo cha Kagoda bado, kiporo cha Deep Green Finance bado na inakuwa mbaya zaidi unapozungumzia Deep Green Finance ambayo imepora dola 10 milioni,” alisema Ole-Sendeka.
“Mbaya sana kampuni hiyo (Deep Green) ilikuwa ni wateja wa kampuni moja ya mawakili maarufu ambao moja kati ya wamiliki ni waziri katika serikali hii, tena mwenye nafasi muhimu ya kuwezesha kupatikana kwa wale wateja wao ili wachukuliwe hatua jambo ambalo litajenga imani ya serikali ya CCM kwa wananchi.”
Aliitahadharisha serikali kuwa ajenda ya kuwasakama na kutaka mafisadi nchini washughulikiwe imekuwa ikipigiwa kelele na wabunge kwa miaka minne iliyopita, lakini kumekuwa hakuna hatua za kuridhisha zinazochukuliwa.
“Ni jambo ambalo tumekuwa tukilizungumza kwa miaka mitatu hivi na nusu na huu ni mwaka wa nne, nalo ni la kuitaka serikali ichukue hatua za makusudi na za haraka kufunga ajenda inayoitwa ya ufisadi. Hili si jambo jema sana kusikika masikioni mwa Watanzania,” alisema Ole Sendeka.
Sendeka hakumtaja kigogo huyo, lakini Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha aliwahi kukiri kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Mwanza mwaka huu kuwa, kampuni yao ya uwakili iliwahi kufanya kazi za Deep Green.
Baada ya kubanwa na wapigakura wake, Waziri Masha alijitetea kuwa hahusiki na ufisadi wa Deep Green, lakini kampuni yao ya uwakili ya IMMMA ilipewa kazi na serikali ya kuifungua na kuifunga kampuni hiyo.
Deep Green, ambayo inahusishwa na CCM, inadaiwa kuhusika katika malipo ya zaidi ya Sh215 bilioni yaliyofanywa na Benki Kuu (BoT) kwa njia ambazo zinatia shaka, sambamba na kampuni za Kagoda, Tangold na Mwananchi.
Akijenga hoja hiyo na kuonyesha jinsi inavyomkera akisisitiza kuwa hayuko tayari kuacha kuibana serikali, Sendeka alinukuu Korani akisema: “Ikiwa kuna jambo linalokukera, unaloamini jambo hili ni kero. Chukua hatua za kuliondoa jambo hilo," alisema.
"Na kama huwezi mshtakie jambo hilo kwa mtu mwenye uwezo na kama hajaweza kuliondoa endelea kwa hasira zako kwa kulinyooshea kidole kulikemea jambo hilo ovu ili hatimaye liweze kuondolewa."
Alisema kuwa ufisadi ni jambo ambalo linamkera na linakikera chama chake cha CCM na lilianza kupigwa vita tangu serikali ya awamu ya kwanza iliyokuwa inaongozwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Alinukuu maneno katika moja ya hotuba za Mwalimu Nyerere wakati mfumo wa vyama vingi unaanza nchini alipoitaka CCM iwaepuke watu waovu na umoja bandia.
“Uking’ang’ania umoja bandia na watu wasio na maadili, utaununua umoja huo kwa kupoteza itikadi yako na itakuwa kama gulio tu la kuwakusanya watu wa kila aina wanaotaka vyeo," alisema.
Kwa mujibu wa Ole Sendeka, wabunge wa CCM wataendelea kupigia kelele suala la ufisadi na hata kama serikali haitekelezi wataendelea kuisakama.
Awali, alisema kuwa mtu anayesema kuwa CCM haijatekeleza ilani yake, anapaswa kuwa na sifa mbili tu.
Moja alibainisha kuwa mtu huyo anapaswa kuikana nafsi yake kwa hatua ambayo mhusika anatakiwa kuheshimu utashi wake kwa kusema ukweli.
“Lakini nyingine ambayo sidhani kwamba inaweza kupatikana Dodoma ni ile ya kuwa na upungufu wa akili, lakini naamini hili haliwezi kutokea hapa kwa sababu (Hospitali ya) Mirembe ipo hapa karibu na tiba yake inapatikana bure.”
Alisema kwamba, Rais Jakaya Kikwete anafanya kazi nzuri ambazo anastahili kupongezwa kulingana na ahadi alizozitoa.
Alijigamba kuwa hata yeye ametekeleza ahadi zake ipasavyo akitoa mfano kwamba alipochaguliwa kuwa mbunge wa Simanjiro mwaka 2000 alikuta shule tatu za msingi na hadi sasa anapotimiza miaka 10 kwenye kiti hicho, anakamilisha shule tatu ili ziwe 17.

No comments:

Post a Comment