.

.

.

.

Wednesday, June 10, 2009

SHAHIDI MWINGINE AFARIKI "KESI YA ZOMBE"

SHAHIDI wa 34 wa upande wa mashitaka katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wa Mahenge mkoani Morogoro na dereva wa teksi, inayomkabili aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Abdallah Zombe na wenzake, Elly Nkya (57), amefariki dunia kwa ajali ya gari. Alifariki usiku wa kuamkia juzi, baada ya gari alilokuwa akisafiria kupata ajali eneo la Kiluvya, mkoani Pwani. Elly alikuwa askari wa Jeshi la Polisi Makao Makuu, mjini Dar es Salaam kitengo cha Upelelezi wa Makosa ya Jinai. Alikuwa mpiga picha wa matukio mbalimbali ya uhalifu yanayohusu upelelezi. Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu Ombeni Nkya(40), dada yake alikufa baada ya gari hilo kupata ajali eneo la Kiluvya, Dar es Salaam, alipokuwa akirejea kutoka Kidatu mkoani Morogoro kwa shughuli za kikazi. Nkya alisema mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kijiji cha Nkoanrua, Arumeru mkoani Arusha kwa maziko inafanyika nyumbani kwa marehemu, Mtoni Kijichi Dar es Salaam. "Mipango ya kusafirisha mwili wa marehemu inaendelea kufanywa hapa nyumbani kwa marehemu na tunachosubiri ni kibali cha mwajiri wake Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, lakini vyovyote itakavyokuwa tunatarajia kuusafirisha kesho (leo) kwenda Arumeru kwa maziko," alisema Nkya. Nkya alisema marehemu ameacha mume Selemani Nyakipande na watoto watano Stellah (21), Zawadi (18), Fredrick (26), William (15) na Adam (11). Marehemu Elly ni miongoni mwa mashahidi waliosisimua katika kesi inayomkabili Zombe na wenzake tisa, kutokana na ushahidi mzito alioutoa. Elly ndiye aliyekwenda eneo la mauaji katika msitu wa Pande na kupiga picha. Katika ushahidi wake alidai aliona mafundo manne ya damu yaliyoganda. Alidai walipelekwa eneo la tukio na mshitakiwa wa 11 Rashid Lema, ambaye naye ni marehemu, na kwamba alishangaa kuona eneo hilo kwani hata yeye mbali na kuwahi alikuwa hapakumbuki. Mbali na Elly wengine waliofariki katika kesi hiyo, ni pamoja na Lema aliyefariki dunia kabla ya kutoa utetezi wake uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu na watu waliokuwa wakihudhuria kusikiliza kesi hiyo. Wengine ni kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Moses Maira, aliyekuwa akimtetea Zombe na mwingine ni mzee wa Mahakama, Michael Gonzaleth.

No comments:

Post a Comment