.

.

.

.

Friday, July 17, 2009

KYELA YAGEUKA IRAN

HALI ya mji wa Kyela na vitongoji vyake si shwari baada ya kundi la wananchi kuvamia Kituo Kikuu cha Polisi kwa lengo la kuwateka askari polisi, waliodaiwa kumpiga hadi kumuua kijana mmoja waliyemkamata kwa tuhuma za uzururaji.
Inadaiwa kuwa kijana aliyeuawa, Lucas Mwaipopo, alifariki akiwa mikononi mwa polisi waliomkamata kwa tuhuma za uzururaji.
Vurugu hizo kubwa zilifikia hatua ambayo wananchi waliamua kuvamia maduka na kupora wakati kundi jingine la wananchi likivamia Mahakama ya Mwanzo ya Kyela mjini, kuchoma moto na kuteketeza chumba cha kuhifadhia nyaraka.
Wananchi hao pia walivamia ofisi ya halmashauri ya wilaya hiyo na kuyaponda vibaya kwa mawe magari yaliyokuwa katika ofisi hizo.
Vurugu hizo zilisababisha shughuli za kibiashara kwenye mji huu kufungwa kwa siku nzima ya juzi huku wafanyakazi wakikimbia na kuziacha wazi ofisi zao kwa kuhofia usalama wao.
Watu saba waliojeruhiwa katika tukio hilo walipelekwa hospitali ya rufaa ambao ni Daud Kibona ambaye risasi ilimvunja mfupa wa mkono, Jacob Anthony aliyepigwa risasi tumboni na ikatokea kwenye makalio.
Wengine ni Yuda Andrew pamoja na Ramadhani Hassan na polisi Koplo Mbaga na Koplo Robert ambao walijeruhiwa kwa mawe katika vurugu hizo.
Hasira hizo zilitokana na wananchi hao kushindwa kumuona mkuu wa mkoa wa Mbeya, John Mwakipesile baada ya kwenda nyumbani kwake ili kutoa malalamiko yao dhidi ya unyanyasaji wa polisi.
Inadaiwa kuwa mkuu huyo wa mkoa alilikwepa kundi la wananchi waliokuwa wakielekea nyumbani kwake na hivyo kuamsha hasira za wananchi walioamua kuvamia kituo cha polisi na kuanza kupambana kwa mawe na askari polisi ambao walijibu kwa kufyatua risasi.
Wakati vurugu hizo zikiendelea, wananchi walichoma moto matairi ya magari na kupiga mawe magari yaliyokuwa yakipita barabarani.
Mapambano hayo baina ya polisi na wananchi yalidumu kwa zaidi ya saa nne wakati polisi walipofanikiwa kurejesha hali ya usalama baada ya kuongezewa nguvu na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliofika eneo la tukio saa tatu baada ya mapambano kuanza.
Msafara wa FFU waliokuwa katika magari matatu uliongozwa na kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Advocate Nyombi .
Katika tukio hilo, watu wanne waliripotiwa kujeruhiwa kwa risasi huku askari kadhaa wakidaiwa kujeruhiwa kwa mawe.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Nyombi aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafikishe malalamiko yao polisi.
Alisema kuwa Jeshi la Polisi litapambana na kuhakikisha kuwa watu walioanzisha vurugu hizo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Alisema kuwa madhara zaidi juu ya tukio hilo yatafahamika baadaye na akaahidi kuchunguza chanzo cha tukio hilo.
Wakizungumza kuhusu uamuzi wao wa kufanya vurugu hizo, wananchi walioonekana kuwa na jazba walisema ulitokana na serikali ya mkoa na wilaya kutotaka kuwasikiliza na kuwapuuza.
Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Edgar alisema kuwa haiwezekani wakapuuzwa kwa jambo zito lililosababisha mwenzao kuuawa kwa makasudi na badala yake serikali iwaone kuwa wananchi ndio hawana maana.

No comments:

Post a Comment