.

.

.

.

Friday, July 31, 2009

SITTA AOMBA ULINZI SERIKALINI


SPIKA wa Bunge Samuel Sitta ameiomba Serikali kumwongezea ulinzi kwa kuwa mafisadi wameongeza nguvu ya vita dhidi yake.
Spika Sitta alisema hayo alipokuwa akizungumzia tuhuma dhidi yake, zilizoripotiwa jana na baadhi ya vyombo vya habari kuwa anafanya njama kuchoma nyaraka za Bunge.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Spika anadaiwa kula njama ili kuchoma ofisi ya mhasibu wa Bunge ili kuharibu nyaraka muhimu zinazomhusisha na ubadhirifu wa fedha za Bunge.
Lakini Spika Sitta alijibu tuhuma hizo bungeni akisema taarifa hizo zina mkono wa wabaya wake, wenye lengo la kumchafua katika utendaji wake.
“Hivi kama kweli nataka kuficha faili la Bunge nani anaweza kunizuia humu ndani?” alihoji Spika Sitta na kuongeza:
“Hizi ni taarifa za wabaya wangu, wanachofanya ni kuziweka kwenye internet kwanza halafu wanazisambaza kwenye vyombo vyao maalum, magazeti manne; gazeti la Tazama, Tanzania Daima na mengine mnayoyaona," alisema Spika na kuongeza:
“Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba mnipe ulinzi zaidi, hii vita ni ngumu na kubwa sasa. Ulinzi mnaonipa naona hautoshi,” alilalamika Spika Sitta na kuwaponda wanaomwandama kuwa hata iweje, ataendelea kushinda ubunge jimboni kwake na kuwa Spika kama bado atakuwa hai mwakani.
Alifafanua kuwa fedha wanazopeleka maadui zake jimboni kwake Urambo zinasaidia kuimarisha maendeleo, lakini hazitomng’oa madarakani.
"Wananchi wangu wanajua ninachokifanya jimboni kwangu, hata wakipeleka pikipiki bado nitashinda," alisema Sitta.
Mara kwa mara Spika Sitta amekuwa akidai kwamba anaandamwa na mafisadi ambao wanataka aache kufichua maovu yao.

No comments:

Post a Comment