.

.

.

.

Wednesday, July 15, 2009

TICTS YABANWA

HATIMAYE serikali imemaliza utata wa mkataba wa Kampuni ya Tanzania International Container Service (Ticts), baada ya kuiondolea ukiritimba wa shughuli za kupakua shehena na makontena katika Bandari ya Dar es Salaam.
Uamuzi huo umefikiwa siku chache baada ya gazeti hili kuripoti kwa mara ya kwanza, kuundwa timu ya mawaziri wanne chini ya Dk Shukuru Kawambwa (Miundombinu), kuibana Ticts ili kuondoa ukiritimba na kuuza asilimia 25 ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku serikali ikijiandaa kutoa ripoti kamili ya utekelezaji kuhusiana na suala hilo Julai 30, mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu, Omar Chambo alilithibitishia gazeti hili jijini Dar es Salaam jana kuhusu uamuzi wa kutaka kuondoa ukiritimba huo wa TICTS.
Hata hivyo, uamuzi huo wa serikali bado haujaanza kutekeleza azimio la Bunge la Aprili 25 katika mkutano wa 11 mwaka jana lililotokana na hoja binafsi ya mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi aliyeitaka serikali kufuta nyongeza ya mkataba kwa Ticts.
Waziri wa zamani wa Nishati na Madini Nazir Karamagi, anamiliki asilimia 30 ya hisa za Ticts kupitia Kampuni ya Harbours Investment Limited (HILI), huku Kampuni ya Hutchison Port Holdings (HPH) ya Hong Kong, China ikimiliki asilimia 70.
"Ndiyo, lengo la kuondoa ukiritimba ndilo jambo kubwa linalopaswa kufanyika," alithibitisha Chambo kwa kifupi na kusema maelezo kuwa wakati huo alikuwa katika mkutano.
Azimio hilo la bunge kutaka kusitishwa kwa mkataba wa TICTS, lilipitishwa karibu na wabunge wote isipokuwa Karamagi, aliyetoa sauti bungeni ya 'siyo' baada ya Spika kuhoji wabunge wanaoafiki na wasioafiki.
Mkataba huo uliongezwa na serikali Desemba 30, mwaka 2005 na kufikia miaka 25 badala ya miaka 10 ambao ulikuwa unaisha mwaka 2010.
Nyongeza ya mkataba kwa miaka 15, ilifanywa kupitia barua Na. TYC/R/160/32 ya Septemba, 2005, iliyoandikwa na kutiwa saini na aliyekuwa Waziri wa Fedha wakati huo, Basil Mramba, ambayo pamoja na mambo mengine, ilimtaka Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) ahakikishe muda wa mkataba unaongezwa kuwa wa miaka 25.

No comments:

Post a Comment