.

.

.

.

Friday, July 03, 2009

UFISADI MAENEO YA HIFADHI YA MIKOKO

ZAIDI ya vigogo 100 wamejimilikisha maeneo makubwa katika hifadhi ya mikoko kando mwa bahari ya Hindi, kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Miongoni mwa vigogo hao, wamo mawaziri wa sasa na wa zamani wa serikali, kampuni za watu wenye asili ya kiasia na wafanyabiashara maarufu nchini. Vigogo hao wamejenga majumba ya kifahari, vibanda vya utalii na mwingine ameweka matuta kuzuia samaki aina ya Chache, ambao huishi katika maeneo ya chumvi chumvi. Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Maliasili na Utalii, imeanzisha kampeni ya kung’oa mawe ya alama za mipaka yaliyowekwa na kuvunja vibanda. Akizungumza juzi wakati wa ziara ya waandishi wa habari kutembelea maeneo hayo, Ofisa Misitu Mwandamizi wa wizara hiyo, Zawadi Mbwambo, alisema maeneo yaliyotwaliwa na watu hao kinyemela ni takriban hekari 100, ambapo kwa Dar es Salaam ni hekari 60 na zilizobaki ni za Bagamoyo, Pwani. Hatua ya kumiliki maeneo hayo alisema ni kinyume cha sheria na kwamba, inahatarisha kutoweka kwa mikoko na viumbe wanaoishi maeneo hayo. Mbwambo alisema vigogo hao wamekuwa wakimiliki maeneo hayo kinyume cha Sheria ya Misitu na. 4 ya mwaka 2002 na Kanuni za Misitu za mwaka 2004. Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 25, sehemu ya pili cha Sheria hiyo, mtu yeyote hawezi kupewa haki ya kumiliki eneo lililotangazwa kuwa hifadhi ya msitu. Hata hivyo, alisema maeneo ya hifadhi ya mikoko mtu yeyote anaweza kupewa iwapo atafuata taratibu za matumizi, ambayo ni kwa ajili ya ufugaji wa samaki, nyuki na uvunaji wa chumvi. Kwa mujibu wa Mbwambo vigogo hao walikwenda kwenye vijiji vya maeneo hayo, kuwarubuni wanavijiji na hatimaye kwenda Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambako walipatiwa hatimiliki bila wizara kuona kama maeneo hayo yamekatazwa kwa kuwa ni hifadhi ya mikoko. Mbwambo alisema baada ya kubaini hali hiyo, wizara iliwafuata maofisa ardhi wa wilaya na manispaa ili kufahamu wamiliki wa maeneo hayo, lakini wamekuwa wakipewa majibu yasiyo ya kuridhisha, ambapo hupewa jina moja la mhusika. “Sijui maofisa ardhi hao wana nini kwa kweli wanatushangaza kwa sababu mtu unapomwambia jina moja atawezaje kumfahamu huyo mtu. Badala ya kutupatia majina yote mawili wanatupa moja… kwa kweli suala hili linakuwa gumu sana, tumeamua kuanza kampeni ya kung’oa alama za mawe,” alisema. Mbwambo alisema kampeni hiyo itakayohusisha kung’oa mawe hayo ya mipaka na kuyahifadhi kwenye ofisi za maliasili itakuwa endelevu kwa kuwa wanataka kuwafahamu wahusika. Mbwambo alisema tayari kuna taarifa 11 katika vituo vya polisi zinazohusu watu kujimilikisha maeneo ya hifadhi. Ofisa huyo alisema wimbi la uvamizi wa maeneo ya hifadhi limekuwa kubwa, ambapo baadhi ya wavamizi wamekuwa wakitengeneza matuta kwa ajili ya kufugia samaki. Alisema miezi miwili iliyopita walikwenda Bagamoyo na kumweleza mkuu wa wilaya kuhusu jambo hilo.

1 comment: