.

.

.

.

Monday, August 03, 2009

NYANI WA AJABU WILAYANI MUHEZA

WAKAZI wa kitongoji cha Maguzoni, wilayani Muheza, juzi walistaajabu ya firauni baada ya kumuona nyani akiwa na nywele za binadamu kichwani pamoja na hirizi kiunoni na miguu ya mbele na nyuma.
Nyani huyo alidaiwa kutokea katika mazingira ya kutatanisha ambapo
wakazi wa eneo hilo walimhusisha na ushirikina wakidai alikuwa akitumika kuiba chakula na fedha za watu madukani na nyumba za watu kimiujiza.
Chanzo cha kukamatwa kwa nyani huyo ambaye alikuwa mkubwa kuliko nyani wa kawaida, huku akiwa na nywele za binadamu kichwani ni baada ya wananchi wa kitongoji hicho kudai kuwa wamekuwa wakifanya kazi, lakini fedha zao hazionekani ambapo baadhi walidai yupo mchawi anazichukua kimazingara.
Kutokana na imani hizo za ushirikina, wananchi hao walichanga fedha kupitia uongozi wa kitongoji hicho na hatimaye kumtafuta mganga wa kienyeji ili afichue wachawi.
Akizungumzia zaidi tukio hilo, mwenyekiti wa kitongoji hicho cha Maguzoni, Abdallahman Kiganga alisema baada ya mganga huyo kufika, aliishi na wananchi na kudai kwamba yupo mtu katika kitongoji hicho ambaye ni mchawi ndiye anayeiba fedha za watu kishirikina baada ya kujigeuza nyani kimiujiza.
Alisema mganga huyo alijigamba kwamba yeye anao uwezo wa kumvuta kwa dawa mchawi huyo huku akishajigeuza nyani usiku.
Kiganga alisema kutokana na uhakika huo kutoka kwa mganga, wananchi walimkabidhi fungu la fedha na kwamba alianza kufanya kazi hiyo usiku kumtafuta mchawi huyo anayejigeuza nyani na kupora fedha za watu kimiujiza.
Alisema mganga huyo alikwenda katika nyumba moja na kufanya dawa zake usiku huo ambazo zilimwita mchawi huyo ambaye alikuwa tayari ameshajigeuza nyani ili aingie kazini kuiba fedha kama kawaida yake.
Kiganga wakazi wa kitongoji hicho waliitana usiku huyo na kumshangaa nyani huyo akiwa na umbo la binadamu pamoja na nywele za binaadamu kichwani na hirizi miguu ya mbele na nyuma ,shingoni na kiunoni huku akiwa anatisha kuwauma wananchi waliyomzunguka.
Hata hivyo wanachi wenye hasira walimshambulia nyani huyo usiku huohuo na kumuua.
Baadhi ya wakazi hawakupenda kitendo hicho kifanyike na walitoa taarifa kituo cha polisi Muheza kwamba kuna mganga anahatarisha kuvunjika kwa amani katika kitongoji hicho.
Kufuatia taarifa hiyo polisi kwa haraka walikwenda katika kitongoji hicho na kumkuta nyani huyo akiisha kufa baada ya kupata kipigo kutoka kwa wananchi.
Inadaiwa mganga aliamua kuingia mitini baada ya kusikia kwamba polisi waliarifiwa juu ya tukio hilo.
Jeshi la polisi lilimchukuwa nyani huyo katika gari na mwenyekiti wa kitongoji hicho Kiganga hadi kituo cha polisi kama ushahidi huku mganga huyo akiendelea kutafutwa.

No comments:

Post a Comment