.

.

.

.

Monday, February 22, 2010

MABADILIKO JESHI LA POLISI

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, amefanya mabadiliko kwa kuwahamisha makamanda wa mikoa mitatu nchini na kuteua mpya mmoja.

Imeelezwa kuwa lengo la hatua hiyo ya IGP Mwema ni kuboresha utendaji na si vinginevyo.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, Abdallah Mssika, amesema kuwa walioguswa na uhamisho huo ni, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza (RPC), Jamal Rwambow ambaye amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam huku nafasi yake ikichukuliwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Simon Sirro.

Mssika aliwataja makamanda wengine walioguswa na uhamisho huo kuwa ni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Liberatus Sabas ambaye katika mabadiliko hayo amehamishiwa Mkoa wa Tanga kuchukua nafasi ya Sirro.

Aidha, IGP amemteua Kamishna Msaidizi wa Polisi, David Misime, ambaye alikuwa Makao Makuu ya Jeshi hilo kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, jijini Dar es Salaam.

Mssika, aliyasema hayo jana jijini Dar es Saalam kwa niaba ya IGP Mwema, wakati akizungumza na gazeti hili kutoa ufafanuzi kufuatia kuwepo kwa taarifa za uvumi kuhusiana na uhamisho wa maofisa hao waandamizi wa Jeshi la Polisi.

Mssika alisema uhamisho huo haumaanishi kuwa makamanda hao wamefanya vibaya kwenye mikoa yao kama baadhi ya watu wanavyoamini.

Alisema kuwa uhamisho huo ni wa kawaida na umekuwa ukifanywa mara kwa mara lengo likiwa ni kuboresha huduma zaidi kwa wananchi.

"Uhamisho huu hauna maana kwamba makamanda hao wameharibu kwenye mikoa yao, bali ni wa kawaida na umelenga kuboresha utoaji huduma kwa wadau wetu. Naomba watu waondokane na fikra potofu kuwa kamanda akihamishwa kutoka mkoa wake basi ameharibu jambo fulani, hii sio kweli," alisema Mssika.

Kamanda Mssika alitolea mfano kwa baadhi ya makamanda waliokwisha hamishwa kwenye mikoa waliyokuwa wakiifanyia kazi kuwa ni Mkuu wa Operesheni Maalum nchini, Venance Tossi, ambaye aliwahi kuwa Kamanda wa Polisi wa mikoa ya Kilimanjaro na Kagera.

Wengine ni Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ambaye awali aliwahi kuwa RPC wa Mbeya.

"Mimi kabla ya kuwa msemaji wa Jeshi hili, niliwahi kuwa Kamanda wa Polisi mikoa ya Lindi, Shinyanga na Msaidizi wa Kamishna mstaafu wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana, hivyo uhamisho wa maeneo yetu ya kazi haukuwa na maana kwamba tuliharibu, bali ni maboresho kama nilivyokueleza hapo awali," alisema Mssika.

Msikka alitoa ufafanuzi huo baada ya gazeti moja katika toleo lake la jana kuchapisha habari ambayo haikuthibitishwa na jeshi hilo, ikisema kuwa Rwambow amehamishiwa Makao Mkuu ya Jeshi hilo kutokana na mauaji ya watu 14 waliouawa na majambazi wilayani Ukerewe, mkoa wa Mwanza, mwezi uliopita ambapo pia watu wengine 17 walijeruhiwa.

Hata hivyo, Mssika alisema kuwa makamanda waliohamishwa wanatakiwa kuhamia kwenye maeneo yao mapya ya kazi mara moja.

IGP Mwema amewahamisha makamanda hao huku wananchi wengi nchini wakilalamikia utendaji usioridhisha wa Jeshi la Polisi hususan baadhi ya askari kujihusisha katika vitendo vya ujambazi.

Mbali na rushwa ambayo inaendelea kuwa kama sehemu ya maisha ya askari wengi, askari kadhaa wamehusika katika mauaji ya raia lakini hadi sasa hawajachukuliwa hatua.

No comments:

Post a Comment