.

.

.

.

Monday, May 17, 2010

MAUAJI YA KUTISHA

Amuua mkewe kwa kumchinja
Amuua mwanaye na mke wa jirani yake kwa kuwalipua kwa risasi
Naye ajimaliza kwa kujipiga risasi

Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kata ya Cheyo katika Manispaa ya Tabora, amefanya mauaji ya kufuru baada ya kumuua mkewe kwa kumchinja na kitu chenye ncha kali.

Katika hali ya kushangaza, baada ya kumuua mkewe, akamuua kwa kuwapiga risasi mtoto wake wa kumzaa pamoja na mke wa askari mwenzake anayeishi jirani na baadaye yeye mwenyewe kujiua kwa kujilipua kwa risasi.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Afisa Mpelelezi wa

Makosa ya Jinai mkoani Tabora, David Mwakiluma, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 2 usiku juzi.

Alimtaja askari aliyefanya mauaji hayo kuwa ni Bonus Hyella (35), ambaye siku hiyo alikuwa zamu kikazi na kwamba kabla ya kwenda kazini mke wake ambaye alikuwa ameachana naye kwa muda alikwenda kumtembelea mumewe na ndipo askari huyo alipomchinja na kumfungia ndani.

Mwakiluma alisema kuwa baada ya mauaji hayo askari huyo alikwenda kazini na akiwa huko aliomba ruhusa kwenda haja huku akiwa na silaha na ndipo alipokwenda kwa askari mwenzake Sajent Sedekia Raphael na kumuua mkewe. Aliongeza kuwa alipotoka hapo alikwenda kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Cheyo, Anna Malila aliyekuwa na mwanawe Evelyne Hemedi, ambaye alikuwa akifanya usuluhishi wa ndoa yao.

Alisema alipofika hapo alimuuliza Malila alipo mke wake (huku akijua kuwa ameshamuua) na alipojibiwa kuwa hawajui akamjeruhi kwa risasi mguu wake wa kulia. Mpelelezi huyo alimtaja mtoto aliyeuawa katika tukio hilo kuwa ni Dorothea Hyella (22) ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha tano Shule ya Sekondari ya Uyui. Aidha, alimtaja mke wa askari mwenzake aliyeuawa kuwa ni Emmaculate Enthoni aliyepigwa risasi na kufa papo hapo.

Alisema kuwa katika tukio hilo, askari huyo alitumia bunduki aina ya SMG ambayo ilikutwa na risasi moja na maganda tisa ya risasi.

Inasadikiwa kuwa risasi 28 zilitumika kutokana na uwezo wa silaha hiyo, huku maaskari waliokuwa wakitafuta mbinu za kumkamata kulazimika kulala chini ili kukabiliana naye.

Katika harakati hizo askari huyo aliwaponyoka na kukimbia hadi nyumbani kwake ambako alijipiga risasi na kumjeruhi vibaya ambapo alifariki jana asubuhi katika hospitali ya mkoa Tabora.

Majeruhi walionusurika katika tukio hilo wamehamishiwa hospitali ya rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment