.

.

.

.

Thursday, August 19, 2010

AFUNGWA MIAKA TISA KWA KUTAKA KUMUUZA ALBINO


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi, Mkoa wa Mwanza imemuhukumu
raia wa Kenya Nathan Mutei (28) kwenda jela miaka tisa ama kulipa faini ya Sh 80 milioni kutokana na kupatikana na makosa ya kusafirisha albino kutoka nchini Kenya kuja kumuuza kwa kiasi cha Sh 400 milioni.

Mutei alihukumiwa adhabu hiyo na hakimu mkazi Angelous Rumisha baada ya kukiri makosa yake muda mfupi tu alipofikisha mahakamani na kusomewa mashitaka saa 8: 46 mchana wa jana.

Hukumu yake ilisomwa kwa muda wa dakika 18 baada ya maelezo ya wakili wa mashitaka kusomwa na hakimu huyo kupitia ikiwa ni pamoja na kumkabidhi Mutei vielelezo vya maelezo yake ili aweze kuhakikisha maelezo yaliyomo ambayo yanaonyesha kuwa alikiri kosa kama ni yake na kwamba ndiye aliyetia sahihi.

Baada ya Mutei kuhakikisha maelezo yake na sahihi kuwa ndiyo na mahakama ilitulia kwa muda wa dakika 35 huku hakimu akiandika na kisha kuomba maelezo ya wakili wa utetezi na utetezi wa Mutei kisha kuanza kumsomea hukumu.


“Kwa kosa la kwanza la kusafirisha binadamu utakwenda jela miaka tisa ama kulipa faini ya Sh80 milioni na kwa kosa la pili utakwenda jela miaka minane na makosa yote yatatumikiwa kwa pamoja hivyo ukilipa faini kwa kosa la kwanza utaendelea na adhabu ya kosa la pili. Mtuhumiwa anaweza kukata rufaa ndani ya siku 45” alihitimisha hukumu yake hakimu Angelous Rumisha.


Mutei alifikisha mahakamani jana na kusomewa mashitaka mawili katika kesi namba 672 ya mwaka 2010 ambapo kosa la kwanza likiwa ni kumsafirisha binadamu kinyume na sheria ya namba 6 ya mwaka 2008 ya makosa ya kusafirisha binadamu na kosa la pili likiwa ni kumteka mtu na kutaka kumuua na kuuza viungo vyake kinyume na kanuni za makosa ya adhabu namba 248 kifungu cha 16, alikubali makosa yote na hivyo kuhukumiwa kwa makosa yote mawili.

Awali akisomewa mashitaka hayo mawili na wakili wa serikali David Kakwaya alisema Mutei alikuja Tanzania kwa mara ya kwanza Juni mwaka huu na kuonana na mganga mmoja wa jadi (msiri wa jeshi la polisi) na kumueleza kuwa alikuwa akiuza viungo vya albino na hivyo kuandaliwa mtego baada ya msiri huyo kutoa taarifa polisi.

Wakili Kakwaya alisema mtego wa awali ambao uliandaliwa na maofisa wa polisi haukuweza kufanikiwa kutokana na Mutei kurudi nchini Kenya ambako alimshawishi
Robinson Mkwama (20) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino) kusafiri hadi nchini Tanzania ambako alidai kuwa alikuwa amemtafutia kazi ya ukondakta wa gari.

“Mnamo Agosti 12 mwaka huu, mtuhumiwa aliondoka Kitale nchini Kenya wakipitia mpaka wa Isibania na kuja Tanzania ambapo akiwa na albino huyo walifikia nyumba ya wageni ya Riverside iliyopo Nyakato Buzuruga na kupanga chumba namba 4. Akiwa nchini aliwasiliana na msiri wa jeshi la polisi (kama mnunuzi) akitaka kumuuzia na ndipo mtego wa polisi ulipoandaliwa” alieleza.

Wakili huyo wa serikali alieleza kuwa Agosti 15 baada ya kuwasiliana na msiri wa jeshi la polisi saa 10 jioni alikamatwa akiwa katika nyumba ya wageni aliyofikia akijaribu kumuuza albino huyo ambapo Agosti 16 mwaka huu alichukuliwa maelezo polisi ambako alikiri makosa na Agosti 17 alifikishwa kwa mlinzi wa amani na kuchukuliwa maelezo yake ambapo pia alikiri kutenda makosa hayo.

Kufuatia kumalizika kwa maelezo hayo hakimu alimuuliza iwapo alisikia mashitaka na maelezo aliyosomewa na yeye kukiri kuwa alisikia na kufafanua kuwa hakuja na mtuhumiwa huku kwa lengo na nia ya kumuua bali kumuuza kutokana na shinda ya fedha.

Baada ya maelezo yake hakimu huyo alisema mahakama ilimtia hatiani mtuhumiwa huyo na kumuomba wakili wa serikali kutoa maelezo ya mwisho na kisha mtuhumiwa kujitetea.

Akitoa maelezo wakili wa utetezi David Kakwaya alisema hakuna kumbukumbu za makosa wala taarifa za kuwa aliwahi kuhukumiwa na kushitakiwa kwa makosa, lakini aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwake kutokana na kuwa kitendo cha kumsafirisha binadamu kwa lengo na nia ya kumuuza ni cha udhalilishaji na sawa na kile cha biashara ya utumwa ambayo ilipigwa marufuku.

Alisema mahakama wakati wa kutoa adhabu hiyo inapaswa kupima na kuangalia madhara ambayo yangetokea kwa mtuhumiwa kutimiza azima yake endapo asingekamatwa kuwa yangesababisha mauaji hivyo kwa ajili ya kukomesha vitendo hivyo na watu wengine wenye tabia kama hiyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali.

Akijitetea baada ya kutiwa hatiani mtuhumiwa Mutei alisema kuwa alitenda kitendo hicho kwa nguvu za kishirikina kutokana na mganga huyo kupa dawa na kumshawishi kumleta alibino huyo ili ampatie fedha, na kuiomba mahakama kumsamehe na kumsafirisha hadi Kenya kwa vile anategemewa na familia ya watoto watano na baba yake alishafariki.

Hata hivyo hakimu alisema baada ya kusikiliza pande zote mbili, utetezi wa mtuhumiwa hauna nguvu kutokana na kuwa kitendo cha kusafirisha binadamu ni kibaya na matukio ya mauji albino yanalidhalilisha Taifa la Tanzania na kwamba mahakama haitamwonea huruma mtuhumiwa itamuadhibu.

No comments:

Post a Comment