.

.

.

.

Sunday, September 26, 2010

SEIF SHARIF HAMAD ALONGA

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amedai kuwa kuna mkakati maalumu ulioandaliwa kwa ajili ya kumchafua ili asiingie Ikulu ya visiwa hivyo.


Katika hatua inayoonyesha kukubaliana na muafaka baina ya vyama vikuu vya upinzani visiwani humo, Seif pia alisema yupo tayari kufanya kazi na mgombea urais kwa tiketi CCM, Dk Ali Mohamed Shein akiwa rais iwapo chama hicho kitashinda au akiwa kama makamu wa kwanza wa rais iwapo CUF itashinda.

Seif, mwanasiasa mkongwe nchini ambaye anawania urais kwa mara ya nne sasa, amesema kutokana na njama hizo wafuasi wa chama hicho sasa hawana budi kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba ili kudhibiti mkakati huo.
"Pamoja na kwamba kuna mpango maalumu umeandaliwa kwa ajili ya kinichafua na kuichafua Zanzibar kwa ujumla, nipo tayari kuilinda nchi hii," alisema Maalim Seif kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Pwani Mchangani wilayani Kaskazini A, Jimbo la Matemwe..

"Katika hili ninawaombeni muanze kufanya kampeni za nyumba kwa nyumba ili tuudhibiti mpango huu.''
Maalim Seif, ambaye ni mmoja wa viongozi wawili waliofanikisha muafaka wa kisiasa unaotaka kumalizwa kwa siasa za kihasama visiwani humo, alifafanua kuwa mpango huo umeandaliwa ili kuzorotesha maridhiano yaliyofikiwa baina yake na Rais Amani Abeid Karume.


"Pia mpango huo umelenga kunichafua kwa kudai kuwa nikiingia madarakani nitavunja Muungano, jambo ambalo si la kweli,'' alisema Maalim Seif.

Seif alisema pamoja na mambo mengine, akiingia Ikulu ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa kama ilivyokubaliwa kwenye muafaka huo na kuridhiwa na Baraza la Wawakilishi, na kwamba atahakikisha kila sehemu ya Zanzibar inawakilishwa katika serikali hiyo.

Akihutubia katika mkutano huo, Seif, ambaye aliwahi kuwa waziri kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alisema ili kuhakikisha analinda umoja wa kitaifa, serikali ya CUF haitakuwa na ubaguzi wa aina yoyote.
"Ili kuondoa matabaka kwa Wazanzibari, nitaunda serikali shirikishi itayoongozwa na utawala wa sheria," alisema.
"Nataka niwe rais wa Wazanzibari wote si rais wa CUF pekee. Sitapendelea upande wowote katika maendeleo, kila kitu kitakuwa sawa," alisema Maalim Seif.


Maalim Seif alisema kama hakuna amani na utulivu ni vigumu kufikia maendeleo na kwamba amani ya kweli ni pale kila mtu anapopata haki yake.

"Kila Mzanzibari ana haki ya kuwa na chama anachokitaka, lakini ajue kwamba bila nchi hakuna vyama, hivyo usalama na amani ya nchi ndio msingi bora mbele yetu,'' alisema
Maalim Seif alisema kiongozi yeyote wa Zanzibar hawezi kuondoa umaskini hadi aangalie mambo ya msingi ya Muungano na kuyapatia ufumbuzi .
"Ili Zanzibar iweze kusonga mbele inahitaji mamlaka zaidi ya kusimamia mambo yake na ili wananchi watoke katika umaskini ni lazima kuwe na nyenzo za kusimamia uchumi,'' alisema.

Aliwaahidi wakazi hao kuwa itaanzisha sheria ya kupambana na rushwa na kuunda chombo cha kusimamia rushwa Zanzibar.


"Ninawaahidi vijana wa wilaya hii mafunzo maalum ya shughuli za utalii ili waweze kufanya kazi hizo ili kuepusha malalamiko ya wenyeji kukosa kazi na badala yake wanapata wageni pamoja na kukuleteeni matrekta ya power tiller, pembejeo bora(mbegu na mbolea) ili mlime kilimo chenye tija,'' alisema.


No comments:

Post a Comment