.

.

.

.

Wednesday, October 06, 2010

OBAMA AAHIDI MISAADA TANZANIA

Mgombea Urais kupitia Chama cha Mpinduzi (CCM), Dk. Jakaya Kikwete, amesema Rais wa Marekani, Barack Obama, ameahidi kuipa kipaumbele Tanzania katika kuipatia misaada kuliko nchi zingine za Afrika.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Iramba Magharibi mkoani Singida katika mkutano wa kampeni. Alisema Rais Obama alitoa ahadi hiyo hivi karibuni katika mkutano wa Umoja wa Mataifa.

Kikwete alisema anajisikia fahari kubwa kuwa Rais wa kwanza wa Bara la Afrika kukutana na Rais huyo wa Marekani na kwamba hali hiyo imetokana na utendaji mzuri wa serikali yake uliomvutia rais huyo ambapo walikutana na kuzungumza mambo mbalimbali.

“Obama alinieleza sababu za kuanza kukutana na mimi na si viongozi wengine wa Bara la Afrika, juzi juzi tena akiwa UN aliahidi kuwa Tanzania itapewa kipaumbele kwa kupata misaada ya Marekani, ndiyo maana nawaambia sisi tunaaminika na tukiahidi tunatekeleza, nawaomba muichague CCM iendelee kuwaletea maendeleo,” alisema Kikwete.

Alisema ingawa Tanzania bado ni maskini lakini maendeleo yaliyopatikana tangu uhuru hayapaswi kubezwa, kwani maendeleo makubwa yamepatikana katika nyanja za miundombinu, elimu na afya.

Kuhusu elimu, Rais Kikwete, alisema CCM iliahidi katika Ilani ya mwaka 2005 kujenga shule za sekondari katika kila kata na imefanikiwa kutekeleza ahadi hiyo, hivyo aliomba achaguliwe kwa muhula mwingine wa miaka mitano.

Alisema upungufu wa walimu umetafutiwa majibu kwani vyuo vikuu vingi hivi sasa vimeanzisha vitivo vya kufundisha walimu na kwamba baada ya miaka mitatu tatizo hilo litabaki kuwa historia.

Alisema walimu wote watakaokuwa wakimaliza vyuo vya ualimu watakuwa wakichukuliwa na serikali na kutawanywa katika shule zote za sekondari hapa nchini.

Mgombea huyo wa Urais kupitia CCM, aliongeza kusema kuwa bajeti ya elimu imeongezwa kutoka Sh. bilioni 669 hadi Sh. trilioni 2.45 na kwamba bajeti hiyo ndiyo kubwa kuliko bajeti zote kwa mwaka wa fedha wa 2010/2011.

Kuhusu uhaba wa vitabu, Rais Kikwete, alisema amewaagiza maprofesa wa Tanzania waandike vitabu na kwamba Wamarekani wamehidi kusaidia uchapishaji hivyo tatizo la vitabu litaisha kuanzia mwakani, kwani kila mwanafunzi atakuwa na kitabu chake.

Alieleza kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) nayo imeahidi kuikopesha serikali ya Tanzania dola za Marekani milioni 90, ambazo zitatumika kujenga maabara katika shule za sekondari na kukarabati maabara za zamani.

Akizungumzia Hospitali ya Wilaya ya Kiomboi mkoani Singida, mgombea huyo wa Urais, alisema serikali itaendelea kuiboresha hadi ifikie viwango vya kimataifa na kwamba itakarabati zahanati na vituo vyote vya afya vilivyopo katika wilaya hiyo.

Wakati huohuo, Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Dk. Jakaya Kikwete, amewataka viongozi wa chama hicho mkoani hapa kuvunja makundi yaliyotokana na kura za maoni ili chama hicho kiweze kupata ushindi wa kishindo wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31.

Dk. Kikwete aliyasema hayo wakati akiomba kura kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Makao Makuu ya Tarafa ya Nduguti, katika Jimbo la Iramba Mashariki, mkoani Singida.

Upepo wa kisiasa ndani ya CCM katika jimbo hilo haujatengemaa vizuri, tangu wakati wa kura za maoni, hali iliyosababisha mpasuko wa kisiasa na hivyo kuipa wakati mgumu CCM kumnadi mgombea ubunge wa jimbo hilo Salome Mwambu.

Katika kura za maoni ndani ya chama hicho zinazoendelea kulalamikiwa na wananchi, Salome, aligombea na wana CCM wengine wanane, akiwemo aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mgana Msindai.

Kutokana na hali hiyo, Dk.Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM aliwaomba wananchi wa jimbo hilo wahakikishe wanawapigia KURA wagombea wa chama hicho tawala pekee, ili waweze kutekeleza vizuri ilani ya chama hicho.

Katika hatua nyingine Dk.Kikwete alisema kuwa CCM imeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zilizopo katika sekta ya elimu iwapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi katika uchaguzi mkuu ujao.


No comments:

Post a Comment