.

.

.

.

Monday, November 29, 2010

MOTO WAANZA WIZARA YA UJENZI

SIKU moja baada ya kula kiapo cha utiifu, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Naibu Dk Harrison Mwakyembe, wameingia wizarani hapo kwa kutema cheche, huku waziri huyo akitishia kutegesha fedha za ‘moto’ Takukuru kunasa vigogo wanaokula rushwa kwa makandarasi.Magufuli waziri mwenye mvuto kwa umma kutokana na utendaji kazi wake wa kasi, uhakika, ufuatiliaji na ujasiri, aliteuliwa kurejea kwenye wizara hiyo aliyowahi kuongoza wakati wa serikali ya awamu ya tatu.

Dk Mwakyembe naye ana rekodi ya upambanaji dhidi ya ufisadi kutokea bungeni ambako aliweza kufichua kasoro za mkataba wa kifisadi wa Richmond Development (LLC).

Akizungumza na watendaji wakuu wa wizara akiwemo Katibu Mkuu na Naibu wake, wakurugenzi na wakurugenzi wasaidizi na wakala wa wizara, katika mkutano wake wa kwanza, Magufuli alizungumzia mambo muhimu saba ambayo yamekuwa ni sawa na donda ndugu kwa wizara hiyo.

Dk Magufuli alitaja mambo hayo kuwa, ni mvutano ndani ya Wakala wa barabara (Tanroads) kufuatia ajira tete ya Ofisa Mtendaji Mkuu, rushwa katika kandarasi, ujenzi wa daraja la Kigamboni, barabara ya Mandela, tatizo la msongamano wa Dar es Salaam na mpango wa ujenzi wa barabara za juu (Flyovers), malipo ya nyumba za serikali, usimamizi wa barabara na kupiga vita makundi na majungu kwenye wizara.

Katika kikao hicho ambacho awali, kilipaswa kuwa cha ndani, lakini Dk Magufuli akaruhusu waandishi kuingia, aliingilia sakata la ajira ya Mrema huku akimshangaa kwa kutoa matangazo ya ajira za Mameneja wote wa mikoa wa Tanroads na wakuu wa idara nyeti makao makuu, bila kile alichokiita idhini ya bodi.

Bila kusita, Waziri Magufuli alimtaka Mrema kusimamisha ajira hizo na kuwaandikia barua mameneja waliopo kuendelea na kazi zao kama kawaida, isipokuwa nafasi moja iliyowazi ya meneja wa Mkoa wa Dodoma.

“Nimesoma katika gazeti moja wiki hii, umetangaza nafasi za kazi…kuna utaratibu kwa kazi zozote zinapotangazwa, hivyo waandikie vyombo vya habari kuwa umefuta nafasi hizo,” alisema Dk Magufuli na kuongeza:
“…umetangaza nafasi hizo baada ya kuona nawe unaondoka, fanya kazi hata kama hiyo nafasi imetangazwa na fanya kama vile hutaondoka kesho na unaishi miaka 100.”

Waziri huyo alielezea kushangazwa kwake pia na ripoti ya Mrema, aliyotoa hivi karibuni ya utendaji Tanroads na kuweka bayana kuwa, ilikuwa na upungufu kwani haikuwa na sahihi ya aliyekuwa waziri wa kipindi hicho, Dk Shukuru Kawambwa, wala Katibu Mkuu wa wizara hiyoi, Omari Chambo.


Dk Magufuli ambaye anaonekana kuwa mkali, jasiri na mwenye msimamo katika kazi, alionya watendaji wote kwa ujumla akiwaambia: “Majungu yaishe kwa kuwa hayatatujenga na tena mmekuwa mkila rushwa kwa sasa tunawaambia, tutategesha hata hela za mapolisi nawaombeni muache rushwa kwa wakandarasi.”

Akizungumzia suala la pili, Dk Magufuli alisema kipindi cha miaka mitatu cha uongozi wake, atahakikisha barabara za juu zimeanza kujengwa kuondokana na msongamano wa magari Dar es Salaam.
Kuhusu ujenzi wa barabara ya Mandela, alitaka taarifa ya mwelekeo wa ujenzi wake ndani ya kipindi cha mwezi mmoja kuanzia jana.

Dk Magufuli kwa msisitizo alisema: “Tumekuja kufanya kazi, wananchi wamechoka kuona ubabaishaji huo, na kuanzia ni barabara ya Mandela, nataka taarifa ya ujenzi ndani ya mwezi mmoja, kwa maana mkandarasi sijui ni rafiki yenu au ni ndugu yenu kwani, hata kituo cha kazi hayupo sasa nataka ripoti yake alipofikia.”

Alisema hakuna haja ya kuwasumbua askari wa usalama barabarani kuongoza msongamano wa magari, huku wakazi wa jiji wakilia na kulalamikia kuhuau kero hiyo wakati nchi imesheheni wahandisi wa kutosha.

Dk Magufuli alisema kama maghorofa yanaweza kujengwa kipindi kifupi, iweje ishindikane kwa barabara za juu.
“Hata barabara za juu zinawezekana, hivyo kazi ya matrafiki ibakie kukaa na kutulindia nguzo zetu na kukamata magari yanayofanya makosa,” alisema.

Alimpa changamoto Chambo, akimtaka kuhakikisha fedha zinapatikana kutoka Wizara ya Fedha kuharakisha ujenzi wa miradi kwani, hawakwenda wizarani hapo kucheza.

Kuhusu tabia ya baadhi ya wakandarasi wa nje kuzorotesha miradi, alisema tabia ya wakandarasi hao kushindwa kufanya kazi na kugeuza eneo hilo kupata faida, imefikia ukingoni na hivi sasa hawatakiwi, wafukuzwe na kung’anyanywa vibali ili wasifanye kazi eneo lote la Afrika Mashariki.

Dk Magufuli alisema lazima kuhakikisha kila mkuu wa idara anawajibu kuwasimamia wakandarasi wa eneo lake na wakishindwa, hatasita kuchukua hatua ikiwemo ya kuwafukuza kazi.

Alionya: “Sisi pia tutakuwa na kazi tutavamia maeneo na tukikuta mmeshindwa kufanya kazi tutafukuza mkandarasi na wewe ukifuata, hatutacheka na mtu tumekuja kufanya kazi maana barabara nyingi zilizo chini ya Tanroads ndizo zenye matatizo, hivyo lazima malengo yatimizwe kipindi cha miaka mitatu.”

Aliweka bayana kwamba, hataki kuwa mnafiki ndio maana ameamua kueleza ukweli na kama huko nyuma kulikuwa na makundi yanatakiwa kumalizwa kila mmoja linatakiwa lianze kubadilika.

Kuhusu mradi sugu wa ujenzi wa daraja la Kigamboni, Dk Magufuli alionyesha kushangaza kuona ujenzi unasuasua na kutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kuweka bayana kama hauwezi, atahakikisha linajengwa kwa fedha za serikali kwa kuomba kutoka Benki Kuu (BoT).

Kuhusu ujenzi wa uwanja wa ndege Songwe, alisema Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA), Prosper Tesha, anapaswa kuhakikisha na kusimamia kukamilika kwa uwanja huo uliopo mkoani Mbeya kutokana na mkandarasi kuchukua muda mrefu.

“Lazima usimamie ukweli….ni suala la kujiuliza kwanini ule uwanja haukamiliki na hauishi, inawezekana mnawabembeleza nini hao wakandarasi? naomba usimwogope mtu, fanya kazi hata siku ukifa amini utakwenda kuwa mkurugenzi mkuu wa viwanja vya ndege mbinguni,” alisema.

Alitaka watendaji kujituma na kurudisha heshima ya wizara hiyo, kuachana na majungu ya kupigana vita, wenyewe kwa wenyewe jambo lililosababisha kila mmoja kuwa na kundi lake.

Alisema ni vema kuhakikisha wale waliokopeshwa nyumba wanalipa madeni na wakishindwa kufanya hivyo, wafikishwe mahakamani ikiwamo kunyang’anywa nyumba hizo kwa kuwa wanasheria wapo, watakaosimamia shughuli hiyo.


Dk Magufuli alikwenda mbali zaidi akitangaza kufanya mbinu za uchunguzi, kubaini utekelezaji sheria akisema: “Magari yanazidisha uzito, ipo siku nitafanya msako wa kushtukiza kwa magari yanayozidisha uzito… nitaingia katika lori moja na kupanda halafu nitajibadilisha kwa kuvaa miwani na kofia ili nikamate wale wafanya kazi wenu wa mizani maana wanachukua rushwa sana.”

Dk Mwakyembe kwa upande wake, alisema inashangaza kuona ufanisi wa kazi wa wizara hiyo umepotea huku ukiwa na doa.

“Sitaweza kusifu vitu ambavyo sio vya kweli, sioni kama ni kituo cha ufanisi tena nasema haya bila kuchakachua maneno, nimekuwa najiuliza ni kirusi gani kimeingia katika wizara hii?” alihoji Dk Mwakyembe.

Dk Mwakyembe alisema kwa sasa wamejiwekea utaratibu wa kutoa taarifa moja isiyopingana, wataongea lugha moja na kuimba wimbo mmoja ili wizara hiyo iweze kuwa sehemu ya kupigiwa mfano nchini.

Uteuzi wa Dk Magufuli na Dk Mwakyembe katika wizara hiyo nyeti, unaangaliwa na wadadisi wa mambo kuwa utatoa changamoto kubwa kwa watendaji ambao idara zao nyingi zinatajwa kuwa na matatizo, huku Idara ya Ufundi na Umeme inayoshughulikia vivuko, ikitajwa na ripoti mbalimbali za serikali inaongoza kwa mafanikio ya ufanisi kiutendaji.

HISANI : MWANANCHI

No comments:

Post a Comment