.

.

.

.

Tuesday, January 18, 2011

MATATIZO YA UMEME HUENDA YAKAWA HADITHI

UMEME nafuu na wa kutosha kiasi cha hata Taifa kuuza mwingine nje unakuja, ikiwa mazungumzo yanayofanywa sasa ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kitaifa wa makaa ya mawe na chuma utafanikiwa.

Mazungumzo hayo kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa ( NDC) na Kampuni ya Sichuan Hongda ya China, yanafanyika baada ya kampuni hiyo kushinda zabuni ya kimataifa ya uwekezaji.

Mazungumzo hayo kwa upande wa Tanzania yanaongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa NDC, Gideon Nassari na Mwenyekiti wa Bodi, Dk. Chrisant Mzindakaya.

Kwa upande wa China, ujumbe huo unaongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la China na Afrika na Mwenyekiti wa Sichuan Hongda, Liu Canglong ambaye aliwasili nchini juzi.

Kampuni hiyo inatarajia kuwekeza zaidi ya dola bilioni 3 za Marekani, na miezi sita baada ya mkataba unaotarajiwa kusainiwa mwezi ujao, itaanza kufua umeme na miezi 12 baadaye au zaidi itaanza uzalishaji wa chuma.

Kwa mujibu wa Nassari umeme utakaofuliwa kutokana na makaa ya mawe ya Mchuchuma ni megawati 600.

Kwa sasa Tanzania katika hali ya kawaida inatakiwa kuzalisha umeme wa megawati 773 sehemu kubwa ukitokana na maji (asilimia 71) wakati matumizi ni megawati 900.

Katika hali ya kawaida, kwa sasa kuna pengo la megawati 200.

Kwa kuingiza megawati 600 katika Gridi ya Taifa, kutakuwa na uzalishaji wa megawati 1,300 na hivyo kufanya ziada ya megawati 400 za umeme.

Wataalamu wa sekta ya nishati waliliambia gazeti hili jana kwamba hali hiyo ya umeme mwingi wa bei nafuu kuingizwa katika Gridi ya Taifa utachangia kupunguza gharama za umeme ambao kwa sasa ziko juu.

Kitaalamu makaa ya mawe ni nishati nafuu zaidi ya pili mbali na maji na mataifa mengi yenye umeme wa uhakika, huwa na mfumo wa kuzalisha umeme kwa makaa ya mawe.

Mataifa hayo ni pamoja na China, India na Marekani, na wataalamu wanasema umeme huo ni wa uhakika zaidi kuliko unaotokana na vyanzo vya mafuta na gesi asilia.

Akiba ya makaa ya mawe nchini inakadiriwa kutosha kutumika kwa miaka 100 na ni tani zipatazo milioni 540.

Akizungumza mapema kabla ya kuanza kwa mazungumzo hayo Canglong alisema watahakikisha mradi huo unakwenda unavyotarajiwa, baada ya kufikiwa kwa maelewano ya
utekelezaji.

Canglong alisema kampuni yake ina matumaini ya kufanya mradi huo mkubwa nchini kuwa wa maana kwa Watanzania na majirani zao, hasa kutokana na historia za China na Tanzania na uhusiano uliopo.

Alisema Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na hali hiyo waliiona tangu walipofika mara ya kwanza mwaka 2006 na ndiyo maana mara ya pili mwaka 2007 walifikia uamuzi wa kusajili kampuni na sasa wapo kwa ajili ya kutekeleza lengo la msingi la uhusiano wa China na Tanzania, kuinua uchumi.

Sichuan Hongda yenye thamani ya biashara ya mwaka uliopita ya dola za Marekani bilioni 40, imeelezwa kuwa kampuni pekee iliyoeleza wazi kuwa tayari kutumia zaidi ya dola bilioni 3 kufanikisha mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Uwekezaji katika mradi huo uliwaniwa na kampuni 49 za Ulaya, Asia na Mashariki ya Mbali.

Dk. Mzindakaya, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao cha ufunguzi, alisema anaamini kampuni hiyo itatekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa na kuiondoa Tanzania katika umasikini uliotawala kwa sasa na kuiweka katika uchumi wa kati hata kabla ya kumalizika kwa utawala wa awamu ya nne.

"Hawa wenzetu wakiamua kitu wanafanya, nia yetu tuzungumze tukubaliane na tuone matunda haya mapema zaidi," alisema Dk. Mzindakaya.

Imani yake hiyo pia iliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa NDC ambaye alisema ana matumaini makubwa kutokana na zabuni iliyotumika kumpata mwekezaji huyo kuwa ya wazi.

Alisema kampuni hiyo ina mtaji mkubwa na teknolojia ya hali ya juu: "Si suala la kuleta zabuni ya chini, bali ni la uwekezaji na ni hawa ambao walikuwa tayari kutumia mabilioni katika mradi huo ambao utachangamsha miradi mingine kama ya usafiri wa barabara na reli".

Pamoja na kuwezesha kupatikana kwa umeme huo, kampuni hiyo itajenga barabara za kuunganisha mradi wa Chuma wa Liganga na wa makaa ya mawe.

Reli pia italazimika kujengwa na kwa mujibu wa Nassari kuna kilometa 300 za reli zinahitajika.

Akizungumzia reli Nassari alisema ni mpango wa NDC kuzungumza na Serikali kuhusu uharakishaji wa miundombinu hiyo, hata ikiwa kwa kuitaka kampuni nyingine kutengeneza reli kwa mfumo wa kibiashara.

Kuanza kwa mradi wa Mchuchuma, kutasaidia kuanza uzalishaji chuma kwa kiwango kikubwa katika machimbo ya Liganga.

Mradi wa Mchuchuma na Liganga ni moja ya miradi ya msingi ya maendeleo katika korido la Mtwara, moja ya mradi mkubwa unaoangaliwa na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
.

No comments:

Post a Comment