.

.

.

.

Friday, January 21, 2011

SELIKALI KUDAIWA MIL.5 NA ABDALLAH ZOMBE


HATIMAYE aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Mohamed Zombe, ametangaza rasmi nia yake ya kuishitaki serikali kwa hoja kuwa ilikiuka sheria na Katiba ya nchi wakati ilipomkamata na kumfungulia kesi ya mauaji.
Zombe alikamatwa mwaka 2006 na kufunguliwa kesi ya mauaji ya watu wanne lakini aliishinda serikali katika kesi hiyo.

Uamuzi huo ameutangaza baada ya siku 90 alizotoa kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumwomba radhi na kumlipa fidia ya sh bilioni tano kumalizika.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Tanzania Daima yaliyofanyika jijini Dar es Salaam jana, kamishina huyo wa zamani kupitia kwa wakili wake, Richard Rweyongeza, alikabidhi notisi hiyo ya siku 90 kwa IGP Mwema Septemba 27 mwaka jana, akisisitiza atakwenda mahakamani iwapo masharti hayo ya kuombwa radhi na kulipwa fidia hayatatekelezwa.

Alisema siku tisini hizo zilimalizika rasmi Desemba 25 mwaka jana huku IGP Mwema na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakiwa hawajamjibu chochote mpaka sasa.

Kwa mujibu wa hati hiyo ambayo gazeti hili linayo nakala yake, Jeshi la Polisi lilikiuka sheria ya Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 inayotaka kabla ya mtu kukamatwa ni lazima aelezwe anakamatwa kwa sababu gani na akifikishwa kituo cha polisi ni lazima ahojiwe na kuchukuliwa maelezo yake ambayo baadaye hutumika mahakamani kama kielelezo.

Mbali na hilo, Jeshi la Polisi lilikiuka pia haki za msingi za binadamu na Ibara ya 15(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inayosomeka kama ifuatavyo:

“Kwa madhumuni ya kuhifadhi haki ya mtu kuwa huru na kuishi kwa uhuru, itakuwa ni marufuku kwa mtu yeyote kukamatwa, kufungwa, kufungiwa, kuwekwa kizuizini, kuhamishwa kwa nguvu au kunyang’anywa uhuru wake vinginevyo, isipokuwa tu-
“(a) Katika hali na kwakufuata utaratibu uliowekwa na sheria.”

Akiongea kwa kujiamini huku akilionyesha gazeti hili hukumu mbalimbali ambazo Mahakama ya Rufaa ilitupilia mbali rufaa zilizokuwa zimekatwa na serikali dhidi ya wananchi walioshinda kesi za mauaji katika mazingira kama aliyoshinda yeye, Zombe alisema serikali kama serikali ni nzuri ila kuna baadhi ya watendaji wana hulka za kinyang’au na hawatimizi wajibu wao kama inavyotakiwa.

“Nafahamu kwamba DPP amekata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyotolewa na Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Salum Massati, ambayo ilituachilia huru mimi na wenzangu tisa….hilo halinitishi.

“Nimewasilisha hati hiyo ya nia ya kutaka kuwashitaki na hawajanijibu, hivyo imeonyesha wazi wapo tayari kwenda mahakamani, na mimi na wakili tupo tayari na muda wowote kuanzia leo tunakwenda Mahakama Kuu kufungua kesi ya kudai sh bilioni tano ikiwa ni fidia ya usumbufu na kunyanyaswa kipindi kile nilipokuwa nakabiliwa na kesi ile ya mauaji.

“Sasa kitendo cha Jeshi la Polisi kunikamata na kunifikisha mahakamani na kwenda kuishi gerezani kwa miaka minne bila kuhojiwa na polisi, je, si ndiyo lilikiuka sheria na Katiba zilizotungwa na Bunge, ambapo na huyu huyu IGP aliapa kuilinda Katiba hiyo?” alihoji huku akionyesha kukerwa na jambo hilo.

Zombe ambaye kwa sasa anafanya shughuli zake zinazomuingizia kipato huko mkoani Morogoro, alisema anataka hilo liwe fundisho kwa Jeshi la Polisi ambalo baadhi ya askari wake wamekuwa wakikiuka taratibu kwa makusudi na kuonea wananchi wasio na hatia.
Agosti 17, mwaka 2009, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu ya kushtusha baada ya kumwachilia huru Zombe na wenzake wanane waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja.

Serikali ilikata rufaa Oktoba 7 mwaka 2009 katika Mahakama ya Rufaa kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachilia Zombe na wenzake.

Akisoma hukumu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Salum Massati, alisema baada ya kupitia ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani hapo, alibaini kuwa serikali ilishindwa kuthibitisha mashitaka na kuwa kamwe mahakama haiwezi kumhukumu mshitakiwa kwa ushahidi dhaifu na wa kusikia kama uliowasilishwa mahakamani hapo, kwani kufanya hivyo ni kukiuka sheria.

Kwamba washitakiwa hao si wauaji na aliliagiza Jeshi la Polisi liwatafute wauaji halisi wa marehemu wale.
Chanzo:Gazeti la Tanzania Daima la Alhamisi, Januari 20 mwaka 2011

No comments:

Post a Comment