.

.

.

.

Thursday, January 06, 2011

WABUNGE WA CHADEMA WASEKWA LUPANGO

Image
Wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Arusha wakiandamana kuelekea kwenye viwanja vya NMC mjini Arusha jana ambapo hata hivyo baadaye polisi waliyazuia maandamano hayo. (Picha na Marc Nkwame)

WABUNGE wanne wa Chadema wamesekwa rumande katika kituo kikuu cha Polisi mjini hapa baada ya kukaidi amri ya Polisi ya kuacha maandamano.

Mbali ya wabunge hao kutiwa ndani pia mke wa Katibu Mkuu wa Chadema Willibrod Slaa, Josephine Mushumbusi, naye amekamatwa na kutiwa ndani huku akiwa na majeraha ya kupigwa na polisi.

Pia wafuasi watatu wa chama hicho walijeruhiwa kwa risasi za moto na polisi waliokuwa wakidhibiti maandamano ya wafuasi hao.

Kabla ya matukio hayo, tangu jana asubuhi hadi mchana ulinzi wa polisi uliimarishwa karibu kila kona za Jiji, lakini wafuasi wa Chadema walikaidi amri ya Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema ya kutofanya maandamano.

Badala yake, wafuasi hao walitii mwito wa Dk. Slaa aliyetangaza kupitia vyombo vya habari kuwa wataandamana licha ya amri halali ya Jeshi la Polisi ya kutoandamana.

Wafuasi hao ambao wote walikuwa na vitambaa vyeupe kichwani na vingine vikubwa vilivyoandikwa ujumbe, mabango na wengine wakiimba nyimbo za kumtukuza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, waliandamana wakielekea uwanja wa NMC.

Katika hoteli ya kitalii ya Mount Meru ambako ndiko viongozi wa juu wa Chadema walikofikia, polisi walilazimika kutumia maji ya kuwasha kutawanya wafuasi hao.

Mbali ya hilo katika Kata ya Sombetini, wafuasi hao waliokuwa na vitambaa vilivyosomeka ‘Meya wa Jiji la Arusha wa CCM ni wa kuchongwa’, mengine yakisomeka: 'Tunataka uchaguzi wa Meya urudiwe’, walitawanywa kwa nguvu.

Hata hivyo polisi, mgambo na askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) walidhibiti kwa asilimia kubwa maandamano hayo licha ya kwamba wengine waliandamana kwa magari yenye bendera za chama hicho ili kuchelea kibano.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobis Andengenye, alipoulizwa kwa njia ya simu kama ana taarifa juu ya matukio hayo, alijibu kwa kifupi kuwa yuko kwenye kikao hivyo hawezi kutoa maelezo hadi baadaye.

Hata hivyo, katika mkutano wa hadhara ambao Slaa alianza kuhutubia saa 6 mchana, aliwataja kwa majina wabunge waliokamatwa, kuwa ni pamoja na wa Hai, Freeman Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Dk. Slaa aliwataja wengine kuwa ni Joseph Selasini wa Rombo, Lucy Owenya wa Viti Maalumu na wa Arusha Mjini Godblles Lema ambao wote wako ndani katika kituo kikuu cha Polisi.

Katibu huyo alisema pia kuwa vijana watatu wa chama hicho walijeruhiwa kwa risasi na waliswekwa rumande walipokwenda kituoni hapo kutaka kuchukua fomu namba tatu ya matibabu - PF3.

Dk. Slaa aliwahamasisha wananchi waliofurika katika mkutano huo kuwa iwapo polisi watagoma kuwaachia huru wabunge, mkewe na vijana waliojeruhiwa, atawaachia wafuasi wa chama hicho mjini hapa, kuamua cha kufanya kwani yeye hatahusika kwa lolote.

“Ninawapa muda polisi kuwaachia viongozi wote wa Chadema walioko ndani na ikishindikana umma wa wakazi wa Arusha utaamua la kufanya na mimi sitahusika na lolote,’’ alisema.

Baadaye amri hiyo ilitolewa na wafuasi hao kuelekea kituo cha Polisi ambako walikumbana na mabomu ya kutoa machozi.

Dk. Slaa alifikia hatua hiyo baada ya kuona hakuna uwezekano wa kuwaachia viongozi hao bila masharti ili warudi kuhutubia wananchi juu ya mustakabali wa kwa nini Jiji la Arusha lina Meya wa CCM.

Baada ya kauli hiyo umati ulielekea katika kituo cha Polisi wakitii amri ya kiongozi wao, lakini ghafla Polisi ilionesha ubavu wake na kumimina mabomu huku mamia ya wafuasi hao wakionesha hofu na kutawanyika hovyo mitaani.

Hali hiyo pia iliwakuta pia waandishi wa habari. Hata hivyo habari zilisema waandishi wanne wanashikiliwa na Polisi kwa kilichoelezwa na Jeshi hilo kuwa ni kushabikia Chadema.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamesema hatua ya Dk. Slaa kuruhusu wafuasi wake kuvamia kituo cha Polisi ili kuwatoa watuhumiwa ni uchochezi usiovumilika, ambao unaweza kuhatarisha maisha ya watu na amani ya nchi kwa jumla.

Hata hivyo, wengine wameomba suluhu ya kudumu ipatikane ili kuepusha umwagaji damu mkoani humo ambao unachochewa na tofauti za itikadi za kisiasa lakini na uchochezi wa wanasiasa.

Wakati huohuo, katika hali isiyotarajiwa, Diwani wa Sombetini kwa tiketi ya CCM, Alphonce Mawazo, alimkana Rais Jakaya Kikwete mbele ya umati mkubwa wa watu kuwa hakumpigia kura bali alimpigia Dk. Slaa.

Mawazo ambaye aliibuka ghafla kwenye mkutano huo na kulazimishwa kupanda jukwaani, alisema yeye ni mwanamageuzi wa kweli na anaikubali Chadema kwa asilimia kubwa na ndiyo maana katika kura ya urais aliipigia Chadema.

Diwani huyo alisema hayo jukwaani alipokaribishwa na Dk. Slaa na kupewa kipaza sauti na kutamka kuwa yeye ni Chadema ‘damu damu’ ndiyo maana alikuwa hapo kusikiliza mkutano huo na kushukuru kupewa nafasi na kueleza azma yake.

Chadema imekuwa ikidai kupitia kwa Dk. Slaa, kwamba halmashauri za majiji ya Mwanza na Arusha; Hai na Kigoma Ujiji, uchaguzi wa mameya ulivurugwa katika mazingira yanayoashiria kuwapo maelekezo kutoka ngazi za juu.

Hivyo chama hicho kutoa masharti kwamba usifanyike uchaguzi wowote wa mameya au wenyeviti wa halmashauri Mwanza, Kigoma/Ujiji, Arusha na Hai.

Pia Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha ajiuzulu kwa madai ya kukiuka kanuni za halmashauri na kusimamia uchaguzi kinyume na taratibu, vilevile kinalalamika kwamba uongozi wa TAMISEMI uliingilia uchaguzi hasa Kigoma/Ujiji, hivyo wahusika wote wachukuliwe hatua.

Chama hicho pia kinaitaka Serikali imchukulie hatua Ofisa Upelelezi wa Arusha kwa madai ya kuingia na kumkamata mbunge ndani ya kikao halali kinyume na kanuni za uendeshaji wa halmashauri, hivyo kinataka ofisa huyo ajiuzulu au aondolewe.

Chadema pia inadai kuwa polisi ni watuhumiwa katika matukio ya Arusha, hivyo kama hakutakuwa na maridhiano Serikali itakuwa imewalazimisha kuchukua hatua.

Hii ni mara ya pili katika kipindi cha chini ya mwezi, kwa wafuasi wa Chadema kukabiliana na Polisi, mara ya kwanza ikiwa ni Desemba 18 Polisi ilipokabiliana na vurugu zilizoongozwa na Mbunge wa Arusha, Godbless Lema.

Katika ghasia hizo, Lema alipigwa na kulazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa matibabu, kabla ya hapo Polisi ilishatumia maji ya kuwasha na mabomu ya kutoa machozi kutawanya wafuasi hao waliokuwa wamezingira Ofisi ya Manispaa ya Arusha.

Vurugu hizo zilitokana na Chadema kususia uchaguzi wa meya na hivyo CCM na TLP kuendelea nao na kumchagua Diwani wa Olorien, Gaudence Lyimo akisaidiwa na Michael Kivuyo wa TLP, ambaye ni Diwani wa Sokoni.

KWA HISANI YA HABARI LEO

1 comment:

  1. Muandishi wa habari hii anaonekana kwa namna fulani ni mtu wa CCM. Tunachotaka sisi ni mabadiliko ya kweli Tanzania sio ushabiki. Hakuna mtu aliyeibuka na kumlaumu Dr. Slaa kama ilivyoandikwa hapa. Slaa is the hero of our country. Had CCM not interfered the election, he (Slaa) would have been the president. We love and cherish him; the second Nyerere.

    ReplyDelete