.

.

.

.

Sunday, January 09, 2011

WAZIRI SITTA AMWAGA UPUPU

KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida Waziri katika Baraza la Mawaziri ameamua kumkosoa mwenzake hadharani kutokana na uamuzi alioutangaza hivi karibuni kwa Taifa.

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ndiye amepata ujasiri huo kwa kumkosoa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kutokana na kutangaza kuilipa Kampuni ya kufua umeme ya Dowans Sh bilioni 94, hatua ambayo anaona hakustahili
kuitangaza yeye.

Sitta alisema hayo jana, baada ya kumaliza kuongoza mahafali ya Shule ya Sekondari ya Dini ya Maranatha iliyoko Mianzini Kata ya Kaloleni jijini hapa.

Alisisitiza kuwa Dowans ni ya wajanja waliocheza ujanja kwenye karatasi na Serikali kuingia
‘mkenge’ kulipa kitu ambacho alikielezea kuwa hakina sababu za msingi.

Waziri huyo alisema Kampuni ya Richmond iligundulika na Kamati ya Uchunguzi ya Bunge iliyoongozwa na Dk. Harrison Mwakyembe, kuwa haikuwa halali lakini inasikitisha kuona na kusikia mbia wake, Dowans amehalalishwa, “kitu hicho ni hatari sana kufanywa na jamii itakuja kutuhukumu kwa hilo.

‘’Mzabuni feki anacheza karata zake na mbia wake Dowans nasi tudiriki kulipa kitu ambacho si halali … kamwe haiwezi kuwa halali katika maisha yote,” alisema.

Sitta alitoa mfano wa mtu ambaye hakumtaja jina, kuwa ana kampuni 17 nchini, lakini jina lake halionekani katika kampuni yoyote na ambaye alidai anacheza michezo michafu na kulipwa mamilioni ya fedha.

Alisema watu hao wapo na wanacheza na karatasi na kuhalalisha kujipatia mamilioni ya fedha za walipa kodi wa nchi hii.

Pia Waziri alisikitishwa na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya ‘kunawa mikono’ mapema na kukubali kuilipa Dowans, hatua ambayo alisema ilimshitua sana.

Alisema kwa jambo zito kama hilo, ni lazima Serikali ingekaa chini na kuliangalia kwa mapana na hata ingewezekana kuitisha kikao cha Baraza la Mawaziri kujadili suala hilo kwa kina na kulipatia ufumbuzi wa pamoja, lakini Waziri Ngeleja amelisema haraka jambo hilo.

Sitta alisema Sh bilioni 94 zingejenga barabara ya lami ya kilometa 100 yenye ubora wa hali ya juu vilevile kwa kujenga shule za sekondari 300 za kidato cha kwanza hadi cha nne.

‘’Naweza kusema wajanja wametuzidi akili na wamefaidi kodi za wananchi kujilipa, lakini elimu bila maadili nchi inaweza kwenda mrama,’’ alisema.

Waziri Sitta alisema kwa sasa huwezi kufanya lolote juu ya malipo ya Dowans kwani ‘’unawezaje kufunga zizi la ng’ombe wakati ng’ombe wote wameshaondoka?’’

Alisema ataendelea kusema ukweli mwanzo hadi mwisho bila kumwogopa mtu na kamwe hawezi kuwa mwongo na mnafiki kwa jambo lolote.

Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) iliamua katika hukumu yake Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) iilipe Dowans fidia ya Sh bilioni 94 kutokana na Tanesco kuvunja mkataba nayo.

Uamuzi huo uliridhiwa na Serikali baada ya Mwanasheria wake Mkuu, Frederick Werema kuipitia hukumu hiyo
na kujiridhisha kuwa ni halali.

HISANI YA HABARI LEO

No comments:

Post a Comment