.

.

.

.

Monday, February 14, 2011

BARAZA LA MAWAZIRI KAMBI YA UPINZANI LATANGAZWA

KIONGOZI wa kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe leo ametangaza Baraza la Mawaziri la Kambi hiyo linalojumuisha wabunge kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pekee.

Mbowe amelieleza Bunge mjini Dodoma kuwa, mawaziri hao wanatoka Chadema tu kwa kuwa mawasiliano na vyama vingine bado hayajakamilika na ni kun aumuhimu mkubwa wa kuwepo mawaziri hao vivuli ili kuisimamia Serikali.

“Kwa kuwa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ndicho kilichotimiza masharti yatokanayo na kanuni ya 14 fasili ya (4) ya kuchagua kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, hivyo basi, mimi nikiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni nimeamua kwa sasa kuunda Baraza la Mawaziri Kivuli kutoka Chadema peke yake” amesema Mbowe.

“Ni matumaini yangu kuwa, hapo siku za usoni na baada ya kuelewana na kuridhiana na wenzetu, nitaweza kuunda baraza litakaloweza kushirikisha vyama vingine kutoka kambi rasmi ya upinzani bungeni” amesema Mbowe.

Amesema, ingawa Serikali ina jumla ya mawaziri na manaibu mawaziri 50, yeye ameteua mawaziri na manaibu wao wasiozidi 29 ili kutekeleza kwa vitendo mwito wa Chadema wa kutaka kuwe na baraza dogo la mawaziri.

“Ieleweke wazi kuwa wasemaji wakuu wa upinzani ni mawaziri wanaosubiri hivyo watafanya ama kuonesha ambayo serikali haikuyaona au imeshindwa kuyatekeleza” amesema.

“Lengo la kuwa na Serikali kivuli ni kuonesha mtazamo wa upande wa pili. Pale utakapohitajika ushauri baraza kivuli litashauri vilivyo na hatutasita kukosoa kwa lengo la kujenga pale inapobidi”amesema Mbowe bungeni.

Katika uteuzi huo, Mbowe amejiteua kuwa Waziri Kivuli wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), na amemteua Silinde Ernest kuwa Naibu wake.

Amemteua Raya Khamis kuwa Waziri Kivuli wa Sera,Uratibu na Bunge,Vicent Nyerere atakuwa Naibu wake.

Esther Matiko ameteuliwa kuwa Msemaji Mkuu katika Wizara ya Uwekezaji na Uwezeshaji,Said Amour Arfi ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Utawala Bora, Mchungaji Israel Ntse anakuwa Waziri Kivuli wa Mahusiano na Uratibu, na Suzan Lyimo ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Mbowe amemteua Pauline Gekul kuwa Waziri Kivuli katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Grace Kiwelu anakuwa Waziri Kivuli atakayeshughulikia mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais.

Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Kabwe Zitto ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli katika Wizara ya Fedha na Uchumi,Christina Mughwai atakuwa Naibu wake. Mbowe amemteua Godbless Lema kuwa Waziri Kivuli katika Wizara ya Mambo ya Ndani, pia Mnadhimu Mkuu wa Upinzani, Tundu Lissu ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria.

Ezekia Wenje ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Joseph Selasini kateuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, na Silvester Kasulumbayi anakuwa Waziri Kivuli wa Maendleo ya Mifugo na Uvuvi.

Profesa Kulikoyela Kahigi ameteuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa kambi ya upinzani katika Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Halima Mdee ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mchungaji Peter Msigwa anakuwa Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, na John Myika anakuwa Waziri Kivuli wa Nishati na Madini.

Mhandisi Slavatory Machemuli ameteuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Ujenzi, Mhonga Ruhwanya anakuwa Waziri Kivuli wa Uchukuzi, Lucy Owenya kateuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara, Christowaja Mtinda anakuwa Waziri Kivuli Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Dk. Mbasa Gervas anakuwa Waziri Kivuli Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Mbowe amemteua Regia Mtema kuwa Waziri Kivuli Wizara ya Kazi na Ajira, Naomi Kaihula kateuliwa kuwa Waziri Kivuli wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Joseph Mbilinyi anakuwa Waziri Kivuli wa Habari, Vijana na Michezo, Mustapha Akunaay anakuwa Waziri Kivuli wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Opulukwa Meshack anakuwa Waziri Kivuli wa Kilimo,Chakula na Ushirika, na Highness Kiwia anakuwa Waziri Kivuli Wizara ya Maji.

No comments:

Post a Comment