.

.

.

.

Wednesday, February 09, 2011

UVUMI WA DAWA ZA UKIMWI KUPEWA MIFUGO

KUTOKANA na kuibuka uvumi kuwa kuna baadhi ya wafugaji wamekuwa wakitumia dawa za UKIMWI (ARVs) kwa ajili ya kuwakuzia wanyama wanaowafuga ili wanenepe, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imelazimika kuunda kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma hizo na kuwasaka wahusika wa vitendo hivyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, tayari kamati hiyo imefanya ziara mkoani Mbeya na kufanya uchunguzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuhojiana na waathirika wa ugonjwa huo, madaktari na watunzaji wa dawa hizo.

Amesema kamati hiyo imeundwa na wataalamu watano kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na wawakilishi wa Mkoa wa Mbeya.

Ameongeza kuwa kamati hiyo mkoani humo imehojiana na waathirika zaidi ya 100 wanaotumia dawa hizo katika vituo vikubwa lakini hakuna hata mmoja aliyeonyesha kutambua matumizi hayo au kuziuza dawa hizo kinyume na matumizi yake.

Katibu huyo amesema pia waandishi wa habari mbalimbali nao walihojiwa na kushindwa kuthibitisha tuhuma hizo.

Hata hivyo, Blandina amewaomba wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa mitaa, dola na vituo vya afya pindi wanapobaini biashara hiyo haramu.

“Matumizi ya dawa hizi yanatakiwa kufanyika kwa maelekezo na usimamizi wa wataalamu kwani inamsaidia mgonjwa kumuongezea kinga ambayo itamlinda dhidi yia magonjwa nyemelezi na si kunenepesha wanyama au ndege kama inavyodaiwa na baadhi ya watu,” amesema Blandina
.

No comments:

Post a Comment