.

.

.

.

Wednesday, March 16, 2011

EDWARD LOWASSA AFIKA KWA BABU LOLIONDO



WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa juzi alipata tiba ya magonjwa sugu inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile katika Kijiji cha Samunge, Tarafa ya Sale, Loliondo, mkoani Arusha.

Lowassa alifika katika eneo hilo mchana akiwa na viongozi kadhaa wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro na Serikali kisha kupata kikombe kimoja chenye dawa kinachotolewa na mchungaji huyo kwa ajili ya tiba.

Tofauti na viongozi wengine, Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), Jimbo linalopakana na Kijiji cha Samunge, alikwenda huko akiwa na viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini na baadhi ya wapigakura wake.

Akizungumza kwa njia ya simu jana, Lowassa alithibitisha kwenda Loliondo na kuwataja viongozi wa dini alioambatana nao katika msafara wake kuwa ni Askofu Msaidizi wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini, Dk Frederick Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Dayosisi ya Kaskazini Kati (Arusha), Mchungaji John Nangole.
Katika ramani ya utendaji kazi ya KKKT, Jimbo la Masai Kaskazini ndipo kilipo Kijiji cha Samunge ambako ni makazi ya Mchungaji Mwasapile.

“Ni kweli, nimekwenda pale na wapigakura wangu pamoja na viongozi wa dini, Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Dk Shoo na Mkuu wa Jimbo la Masai Kaskazini, Mchungaji Nangole,” alisema Lowassa na kuuliza: “Kwani hiyo nayo ni habari jamani?”

Baada ya Lowassa kufika katika kijiji hicho akiwa na ujumbe wake, aliongoza moja kwa moja hadi kwa Mchungaji Mwasapile na kuzungumza naye kisha akapata kikombe cha tiba na kuondoka.

Kabla ya Lowassa kwenda kupata tiba, amekuwa akitoa msaada wa nauli kwa wagonjwa mbalimbali wa jimbo lake kwenda kwa mchungaji huyo ambaye dawa yake inadaiwa kutibu magonjwa ya saratani, kisukari, pumu, shinikizo la damu na Ukimwi.


Lowassa ni miongoni mwa wanasiasa maarufu nchini ambao wameshafika kwa mchungaji huyo kupata tiba hiyo wakiwamo mawaziri, naibu mawaziri, wabunge, wakuu wa mikoa na wilaya.

Katika jitihada za kudhibiti usalama na kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma kwa mchungaji huyo bila matatizo, Serikali imeimarisha ulinzi kwa kuweka askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), katika kijiji hicho na kusimamia magari. Pia imepeleka wauguzi kusaidia wagonjwa mahututi kabla ya kumfikia mchungaji na imetoa pia jenereta kwa ajili ya kufua umemeKaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raymond Mushi alisema jana kuwa, sasa walau hali ni nzuri kwani msongamano umepungua.


"Ni kweli sasa hali inaridhisha na jana watu wamekwenda kupata tiba na kurejea makwao mapema hili ndilo serikali inalolitaka. Tunaomba watu wanaopeleka wagonjwa wawe wanauliza kwanza hali ya msongamano," alisema Mushi.Mushi alisema inawezekana watu wanaokwenda katika kijiji hicho kusubiriana katika Mji wa Mto wa Mbu ambako kuna huduma nyingi muhimu kuliko wote kwenda huko kwa wakati mmoja.

Alitoa wito kwa watu wenye wagonjwa mahututi kuacha kuwapeleka moja kwa moja kwa mchungaji huyo kabla ya kupata ushauri wa kitaalamu kuhusu afya zao.Katika hatua nyingine, wagonjwa kadhaa waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wameanza kutoroka wodini na kwenda Loliondo kupata matibabu ya magonjwa sugu yanayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile, Mwananchi imeelezwa.


Habari zilizopatikana hospitalini hapo jana zimeeleza kuwa wagonjwa hao walianza kuondoka Muhimbili juma lililopita baada ya Serikali kubariki matibabu hayo. Ofisa mmoja mwandamizi wa hospitali hiyo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, amesema kuwa wakati baadhi ya wagonjwa hao wakiwa wanatoroka wodini, wengine wamekuwa jasiri kwa kuwaaga madaktari wao.

“Wagonjwa wameanza kuondoka na wengine bila hata ya kuaga, hivyo hatujui hatima yao kama watafika salama huko Loliondo,” alisema.Ofisa huyo alisema juma lililopita, mgonjwa mmoja aliyekuwa amelazwa chumba namba 15 katika Wodi ya Kibasila, aliondoka baada ya kusikia taarifa kuhusu huduma hiyo.

“Kuna mgonjwa mmoja aliyekuwa amelazwa Kibasila Wodi namba 15 aliondoka aliposikia kuwa Babu ameanza tena kutoa matibabu hayo ambayo awali yalisitishwa,” alisema.Hata hivyo, Ofisa Habari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaisha alisema hana taarifa za kutoroka wodini kwa wagonjwa hao na kwenda kufuata tiba huko Loliondo... “Sina taarifa zozote za kuondoka kwa wagonjwa hapa hospitalini.”

Matibabu Loliondo yapandisha nauli Ubungo
NAULI za kwenda Arusha kutoka Ubungo, Dar es Salaam zimepanda kwa kasi katika siku za hivi karibuni kutokana na wingi wa wasafiri wanaoelekea Loliondo kupata tiba hiyo ya magonjwa sugu.Habari zilizolifikia gazeti hili jana kutoka kituoni hapo zimeeleza kuwa, nauli hizo zimepanda kutoka Sh18,000 hadi Sh30,000 tangu juma lililopita.


Mmoja wa mawakala wa mabasi ya abiria katika kituo hicho ambaye hakutaka kutajwa gazetini alisema ongezeko hilo la nauli limetokana na baadhi ya mawakala kukodi mabasi na kuwasafirisha abiria.“Nikupe siri moja tu ambayo inatufanya tupandishe nauli. Lengo letu ni kupata faida, ujue sisi tunakodi basi zima kisha tunakatisha tiketi kwa bei yetu ili na sisi tupate faida,” alisema.

Mmoja wa abiria aliyekuwa akisafiri kuelekea Arusha, Charles Manyama alisema mabasi yaendayo huko yamegawanyika katika madaraja matatu yale ya bei ya juu, bei ya kati na bei ya chini lakini kwa sasa bei imekuwa ni moja kwa mabasi yote.


Kwa mujibu wa abiria huyo, zamani nauli za Arusha zilikuwa Sh25,000 kwa basi la daraja la juu, Sh18,000 kwa mabasi ya daraja la kati na Sh15,000 kwa daraja la chini, lakini sasa mabasi yote yanatoza kati ya Sh25,000 hadi Sh30,000.“Mawakala hawa wanadhani kila mtu anayepanda magari haya anakwenda Loliondo lakini siyo kweli, wengine tuna safari nyingine kabisa," alisema Manyama na kuongeza:

"Unakuta bei zinashangaza na kupanda sana. Hata hivyo, inashangaza kuona wanadamu tunakosa utu. Watu wanakwenda kupata matibabu wanapandishiwa nauli, walipaswa kuwaonea huruma wagonjwa hawa,” alisema Manyama.Jitihada za kumtafuta Meneja wa kituo cha mabasi Ubungo ziligonga mwamba baada ya taarifa kutoka ofisi kwake kueleza kuwa alikuwa nje kikazi.

Polisi Arusha wadhibiti usafiri wa Loliondo
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha limeitaka Halmashauri ya Jiji la Arusha kuweka vituo vinavyotambulika kwa ajili ya wagonjwa wanaokwenda kupata matibabu kwa Mchungaji Mwasapile ili kuepuka utapeli.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alisema jana kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu kutaka kwenda Loliondo, kumezuka vituo vingi ambavyo vinaweza kuwa chanzo cha utapeli kwa watu wanaotoka mikoani."Nafahamu hili ni jambo ambalo manispaa wanahusika nalo, wahakikishe kuwa hakuna vituo visivyo rasmi ili wananchi wasije kudanganywa na watu wabaya," alisema.

Katika kituo kilichoibuka ghafla baada tiba ya magonjwa sugu kuanza kutolewa cha Chini ya Mti, kulizuka vurugu za madereva na madalali waliokuwa wakibishania kiwango cha nauli, hatua iliyosababisha polisi wenye silaha kupelekwa katika eneo hilo.


Hatua ya polisi kuonekana katika kituo hicho, ilisababisha wasiwasi kwa wananchi kuwa huenda Serikali imesimamisha utaratibu wa wananchi kwenda Loliondo, jambo ambalo kaimu kamanda huyo alilikanusha.

"Tunachokifanya ni kuweka utaratibu mzuri, polisi wanasimamia sheria. Magari mengine yanazidisha idadi ya watu na kutoza pesa nyingi zaidi. Sumatra wakisema nauli sahihi ni kiwango fulani na madereva wakizidisha basi tunawakamata," alisema.


Wananchi waliozungumza bila kutaja majina yao walisema kuwa wanashangazwa na bei ya nauli kuwa juu hata baada ya Serikali na KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati kuboresha mazingira ya kuwahi kupata tiba na kuondoka kijijini Samunge.

"Mwanzoni walikuwa wanasema magari yanakaa sana huko, kwa hiyo wanafidia hizo siku za kungoja wagonjwa lakini sasa hivi ukienda leo unarudi kesho na nauli bado iko juu," alisema mmoja wa wananchi hao.Nauli ya kutoka Mjini Arusha hadi Samunge, Loliondo ni Sh100,000 kwenda na kurudi kwa magari aina ya Land Cruser ,huku nauli ya mabasi ikiwa pungufu zaidi.



Habari hii imeandaliwa na Nevile Meena, Ibrahim Yamola, Dotto Kahindi Dar na Mussa Juma, Filbert Rweyemamu, Arusha

No comments:

Post a Comment