.

.

.

.

Monday, March 07, 2011

WAKE WA RAIS JACOB ZUMA WAZIDI KULA BINGO


KAMATI ya Ulinzi wa Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma imetangaza zabuni ya kukodisha magari saba ya kifahari kwa ajili ya wake wa rais huyo. Taarifa zilisema magari hayo yatasambazwa katika miji saba ya Afrika Kusini ukiwemo mji anaotoka Jacob Zuma wa KwaZulu-Natal, kutakuwepo na gari moja ambalo litakuwa tayari kwa ajili ya mke atakayekuwa kwenye msafara kwa siku hiyo.

Kwa mujibu wa nyaraka za zabuni ya kukodisha magari hayo, magari yanayohitajika yanatakiwa yawe ni magari mapya ya kifahari.

Taarifa ya zabuni hiyo pia imeainisha magari yanayotakiwa kwamba yasiwe nje ya magari aina ya Mercedes-Benz S600, BMW 7 series, Audi A8 au A6, Mercedes-Benz ML, BMW X5 series, Audi Q7, Toyota Prado, Toyota Land Cruiser au Nissan Pathfinder.

Mke wa kwanza wa Rais Zuma ni Sizakele Khumalo (67) ambaye anaishi kijijini kwake Nkandla. Wengine ni Nompumelelo Ntuli (34), ambaye alimuoa mwaka 2007.

Mwingine ni Kate Mantsho Zuma raia wa Msumbuji ambaye alijiua mwaka 2000, na wa nne ni Nkosazana Dlamini Zuma ambaye alimpa talaka mwaka 1998, ingawa mtalaka huyo bado ni mshauri wa karibu wa kisiasa wa Zuma na ni Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali yake.

Ingawa wakati wa kuapishwa kuwa Rais, wake watatu walikuwepo, lakini mke wa kwanza tu ndiye aliyemsindikiza Zuma kuingia Ikulu.

Hivi sasa Zuma anaishi na wake zake watatu Gertrude Sizakele, Nompumelelo Ntuli (MaNtuli) na Thobeka Stacie Madiba.

Taarifa zingine zilisema hivi Rais Zuma ana wachumba wawili ambao amepanga kuwaoa katika siku za karibuni. Rais Zuma kwa sasa ana watoto 19.

Utamaduni wa kuoa wake wengi bado una nguvu katika maeneo ya vijijini ya jimbo la KwaZulu Natal, ambako Zuma ametoka.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa mambo ya siasa za nchi hiyo, Protas Madlala, watu wengi wanaotokea katika kabila la Zulu ambao waliamua kuwa Wakristo, wameachana na utamaduni huo wa kuoa wake wengi.

No comments:

Post a Comment