Baada ya dereva wa lori hilo kulisogeza katika nafasi aliyoelekezwa, nasikia sauti ya mmoja wa wahudumu akimwelekeza mwenzake, “…waulize wako wangapi hao?” Mara sauti ya pili inajibu, “wameshasema, wako 58 na watoto 10, leteni dawa… wanywe, waondoke…,”.
Mara masinia yenye vikombe ambavyo idadi yake ni sawa na ya watu 68 walioko ndani ya lori lile vinapelekwa, kisha kugawiwa ndani ya lori hilo.
Katika muda usiozidi dakika 15, watu wote ndani ya lori lile walikuwa wamekunywa dawa. Mmoja wao aliyeonekana kama kiongozi alikabidhi fedha ambazo ni Sh500 kutoka kwa kila aliyekunywa kikombe cha Babu.
Mmoja wa wahudumu wa Babu, anapokea fedha na kusema, “…haya jamani, safari njema.” Lori linaanza kuondoka taratibu huku baadhi ya vijana wakiwa wamening’inia nyuma yake.
Vigelegele baada ya kunywa dawa
Wakati lori hilo likianza kuondoka, mambo makubwa mawili yanajitokeza. Kwanza ni vigelegele na nyimbo za furaha kutoka katika kundi mojawapo na pili ni huzuni na uchungu kutoka katika kundi jingine la watu waliofika kunywa dawa hiyo.
Nyimbo na vigelegele vilivyosikika kutoka ndani ya lori, viliashiria kwamba watu hao walifurahia kutimiza lengo lao, kupata kikombe cha Babu.
Vigelegele hivi vilinipa kishawishi cha kutaka kujua kulikoni? Nilitaka pia kufahamu muda ambao wametumia tangu walipoanza safari, hadi walipofika kwa Babu, Samunge kupata kikombe.
Kutokana na ubovu wa barabara na wingi wa watu katika eneo hili, lori linaondoka taratibu sana hivyo kunipa fursa ya kupenya na kulifikia. Niliwauliza vijana walioning’inia nyuma mahali walikotoka na muda ambao wamekuwa njiani hadi walipofika kwa Babu.
“Wee acha tu mjomba, sisi tumetoka Mwanza, lakini humu ndani wamo watu kutoka Geita, Mugumu, Serengeti na maeneo mengine mengi njiani tulikopita….”
Kwa mujibu wa kijana huyo ambaye sikuwa na muda wa kumwuliza jina lake, walilazimika kusubiri siku nane hadi kufanikiwa kupata kikombe.
Muda wa safari yao ulikuwa zaidi ya saa 36 na siku sita na nusu zilizobaki, zilipita wakiwa kwenye foleni. Kauli hii ilikuwa hitimisho la fikra zangu hasa kuhusu sababu za nyimbo na vigelegele kutoka kwa watu hawa.
Machozi na huzuni
Jambo la pili ambalo lilijitokeza ni kwamba wakati lori hili likiondoka, kulikuwa na gari dogo aina ya Prado lililokuwa na watu wasiozidi 10, likisubiri zamu ya watu wake kunywa dawa. Lakini mkono wa mmoja wa askari waliopo eneo hili ulikuwa juu, ukiashiria lisisogee.
Wakati nikitoka kuzungumza na abiria wa lori lililoondoka nilikuta mkono wa askari huyu ukiwa bado juu, kwa maana kwamba hakukuwa na gari jingine lililoruhusiwa kusogea.
Baada ya muda, kama wa dakika tatu hivi, Fredrick Nisajile ambaye ni msaidizi wa karibu wa Mchungaji, Mwasapila alisema: “…Inabidi tufunge, hadi kesho maana dawa imetuishia.”
Wakati Nisajile akitoa kauli hii, kwenye sinia kulikuwa na vikombe vinne tu vya dawa. Hapo mhudumu aliyekuwa na vikombe vile aliwauliza baadhi ya vijana waliokuwa karibu: “Nani hajanywa dawa? Chukueni hii hapa..” Mara walijitokeza vijana watatu wa kiume kila mmoja akachukua kikombe cha dawa na kubakiza kikombe kimoja.
Baada ya hapo, alitokea mwanamke ambaye alionekana mwenye shauku ya kitu fulani na kwa haraka alichukua kile kikombe kilichobaki na kunywa ile dawa. Huo ukawa mwisho wa utoaji wa dawa siku ile. Ilikuwa saa 2.34 usiku.
Nisajile alichukua kipaza sauti na kuwatangazia watu kwamba muda wa Babu kupumzika ulikuwa umefika na kwamba utoaji wa dawa ungeendelea kesho yake.
Kauli hii ilinifanya nilisogelee kwa taratibu gari lile aina ya Prado ambalo ilikuwa ni zamu ya watu wake kunywa dawa. Katika gari hilo ambalo dereva wake alikuwa ni mwanamke, watu waliokuwamo ndani walikuwa wenye huzuni kubwa. Nilisita kuzungumza nao, maana nilihisi sitapata majibu mazuri kutoka kwao.
Lakini shauku ya kitaaluma ilinituma kujipa moyo, hivyo nilisogelea lile gari, upande alipokuwa dereva na kuwaambia kwa sauti ya chini kidogo… “Poleni jamani.”
Ukimya ulipita kidogo na yule mama (dereva) alionekana kama hapendi kujibu, lakini mtu aliyekuwa kushoto kwake mbele kwa maana ya upande wa pili wa gari alinijibu asante sana.
Kisha alitumia fursa hiyo kutaka kujua kitakachoendelea kesho yake, kwa kunidhania kwamba mimi ni mmoja wa watu wanaotoa huduma ya tiba. Hapo alifungua mlango wa mazungumzo baina yake na mimi ambayo yalichukua takriban dakika nane.
Hapo nikabini kwamba, kama ilivyokuwa kwa lori lililoondoka, pia ilikuwa siku ya nane kwa watu hao walioniambia kwamba wanatokea Dar es Salaam kusubiri kupata dawa. Lakini kubwa ni kwamba matumaini ya kuondoka siku ile hayakuwapo tena na walilazimika kusubiri hadi siku ya tisa.
Kwao ulikuwa ni uchungu, sura zao zilieleza bayana uchungu huu. Yule mama dereva ni kama alikuwa akilengwalengwa na machozi, lakini hakuwa na jinsi ya kubadili ratiba ya siku ile kwani dawa ilikuwa imekwisha.
Macho yaliyojaa shauku
Baada ya pilikapilika za usiku ule, asubuhi yake tulijihimu ili kuwahi miadi baina yetu na Mchungaji Mwasapila kwa ajili ya mahojiano. Wakati mimi na wenzangu, Mussa Juma na Fidelis Felix tukifika nyumbani kwa Mchungaji saa 12.00 asubuhi, tayari makazi yake yalikuwa yamezingirwa na umati wa watu.
Katika umati ule, karibu kila uliyemtazama machoni ungeweza kuona akiwa na shauku fulani. Macho yote yalielekezwa kwenye mlango wa kibanda anamolala Mchungaji Mwasapila.
Hali hii inanipa fikra kwamba, watu hawa ama walikuwa wakitaka kumwona kwa macho yao Mchungaji huyu au walikuwa wakisubiri kuanza kwa ugawaji wa dawa.
Baada ya muda takriban dakika 13 hivi,Nisajile alifika na baada ya kusalimiana nasi, alituambia tusubiri kidogo kwani Babu alikuwa kwenye maombi.
Katika muda mwingine wa dakika kama nne hivi, mlango wa kibanda hiki unafunguka na taratibu anatokea Mchungaji Mwasapila akiwa amevalia kotii la bluu.
Hapo nilianza kuona kila mmoja katika umati wa watu uliozunguka eneo la mbele la makazi yake, akianza kuhangaika kutafuta sehemu ambayo anaweza kumwona vizuri.
Wapo waliohama nafasi zao wakijaribu kupata nafasi nzuri zaidi ya kumwangalia. Kila jicho lilikuwa na shauku ya kufuatilia nyendo zake, ijapokuwa haikuwa rahisi kwani hakuna aliyeruhusiwa kusogea hata hatua moja zaidi ya pale alipokuwa amesimama.
Walinzi walifanya kazi ya kudhibiti uingiaji wa watu katika eneo hili la makazi ya Mwasapila.
Katika pilikapilika zile nilianza kusikia minong’ono kutoka kwa baadhi ya watu: “…Jamani ndiye yule mzee, jamani Mungu ambariki sana, anafanya kazi sana, umemwona ni yule ambaye amevaa jaketi la bluu, yule ni yule pale……”
Kauli hizi zilithibitisha mawazo yangu kwamba kubwa ya yote, watu hawa walikuwa na shauku ya kumwona Mchungaji Mwasapila kujua ni mtu wa namna gani, pengine kutokana na sifa zake kusambaa kwa haraka.
Pengine si rahisi kufahamu kwa nini Watanzania wengi wamekuwa na shauku, pia matumaini katika tiba anayotoa.
Vigelegele, huzuni vya usiku ule na hata umati wa watu ambao ulikuwa nyumbani kwake alfajiri, ni matukio yanayothibitisha shauku hii.
Wengi wanaofika Samunge wanafuata tiba na wengine wana matumaini ya kupona magonjwa yanayowasumbua, pengine baada ya kuugua kwa muda mrefu bila kufanikiwa kupata tiba muafaka.
Lakini unapotazama mchakato mzima wa utoaji wa tiba na kumsikiliza Mchungaji Mwasapila, utabaini kwamba suala la kupona kwa wale wanaokwenda Samunge kupata tiba ni la kiimani zaidi kuliko utaalamu wa kitabibu.
No comments:
Post a Comment