.

.

.

.

Wednesday, May 18, 2011

ZITTO KABWE AZURU KABURI LA AMINA CHIFUPA


MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema juzi alizuru kaburi la Mbunge wa zamani wa Viti Maalumu-Vijana wa CCM, marehemu Amina Chifupa, katika Kijiji cha Lupembe, Iyanjo, wilayani Njombe.

Zitto alizuru kaburi hilo akiwa katika ziara ya mikutano ya hadhara ya Oparesheni Sangara na maandamano ya chama chake, ambayo sasa ipo katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, ikiwa na lengo la kupinga ongezeko la gharama za maisha. Jana alikuwa akitembelea Jimbo la Njombe Kaskazini kufanya mikutano katika vijiji vya Lupembe, Kidegembye na Mtwango.

Kabla ya kuanza mkutano wa kwanza katika Kijiji cha Lupembe, Zitto aliyeambatana na wabunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Raya Ibrahim Khamis na Joyce Mukya waliamua kwenda kuzuru kaburi la marehemu Amina kwa ajili ya kumwombea dua.

Amina alifariki dunia Juni 26, 2007 na kuzikwa Juni 28 mwaka huo kijijini hapo mkoani Njombe.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lupembe, Zitto alisema: "Nashukuru sana kufika katika kijiji chenu kwani nimefarijika kufika mahali alipozikwa marehemu Amina Chifupa".
"Amina alikuwa rafiki yangu sana, tulikuwa tukipambana katika Bunge la 9 la Jamhuri ya Muungano katika kutetea haki za vijana wa nchini."

"Kwa bahati mbaya sikupata nafasi ya kushiriki katika mazishi yake, leo ndiyo mara yangu ya kwanza kufika kaburini kwake," alisema Zitto.

Wakati wakiomba dua kaburini hapo, Mukya alishindwa kujizuia na kuanza kutokwa na machozi huku akisema: "Kwa kweli sitamsahau Amina kwa mambo matatu. Alikuwa mjasiri, mwenye upendo na alijitolea kuisaidia jamii pale alipotakiwa kufanya hivyo au kwa ridhaa yake mwenyewe."

"Amina alikuwa mpambanaji bungeni japokuwa alikuwa na umri mdogo kuliko wabunge wote, aliweza kujitoa kupambana na wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya bila woga."

Source:Mwananchi

1 comment:

  1. Nashukuru kama bado unamkumbuka kwani ulishawahi kula enzi za uhai wake

    ReplyDelete