.

.

.

.

Saturday, December 31, 2016

SIJAWAHI KUOMBA TALAKA - Leyla Rashid




MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Leyla Rashid amesema kamwe hajawahi kuomba talaka kutoka kwa mumewe, Mzee Yusuph.

Aidha, Leyla amesema anajisikia upweke kuendelea kuimba nyimbo za muziki huo bila kuwa karibu na Mzee.

Leyla alisema hayo hivi karibuni, baada ya kudaiwa kuwepo na shinikizo la kumtaka aachane na muziki huo na kuungana na mumewe, ambaye kwa sasa ameacha kuimba taarab na kuwa alhaji.

Hivi karibuni, dada wa Mzee Yusuph, Khadija Yusuph, alikaririwa akisema kuwa, Layla anafanya makosa kuendelea kuimba taarab wakati mumewe ameachana na muziki huo.

Khadija alisema kwa mujibu wa sheria za dini ya kiislamu, mke anapaswa kufuata maelekezo ya mumewe iwapo amemtaka kuachana na fani ambayo yeye ameshaiacha.

Akijibu tuhuma hizo, Leyla alisema ni kweli amewahi kugombana na mumewe mara kadhaa, lakini kamwe hakuwahi kuomba talaka.

Pia, alisema sio kweli kwamba Mzee aliwahi kumtishia kwamba atampa talaka iwapo hataacha kuendelea kujihusisha na muziki huo.

"Hajaniambia acha, isipokuwa mimi mwenyewe najihisi kupungukiwa na kitu fulani.Nilizoea tunakuwa pamoja stejini, lakini sasa hayupo tena,"alisema Leyla.

Mwanamama huyo alisema hadi sasa hajaamua nini la kufanya, bali anamuachia Mungu na kusisitiza kuwa, ni kawaida kwa binadamu kutokosa la kusema, lakini hababaishwi na maneno yao.

"Kama mtu anasema, mwache aseme, mdomo ni mali yake," alisema mwanamama huyo mwenye watoto wawili na kusisitiza kuwa, muda wa kuachana na muziki huo ukifika, atafanya hivyo.

Leyla alisema mumewe hadi sasa hajaonyesha shaka yoyote kwake kwa uamuzi wake wa kuendelea na muziki huo, zaidi ya kumtia moyo na kufuatilia maendeleo yake kila anaposafiri mikoani kwa maonyesho mbalimbali.

No comments:

Post a Comment