.

.

.

.

Thursday, June 16, 2011

AJIFUNGUA MAPACHA WANNE

MKAZI wa mtaa wa Sima kitongoji cha Butiama mjini Bariadi mkoani Shinyanga, Mlinda Shineneko (29), amejifungua salama watoto wanne pacha katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi iliyopo Somanda mjini Bariadi

Muuguzi wa zamu katika hospitali hiyo, Agnes Nyanguleta amesema leo kuwa, Mlinda alifikishwa katika hospitali hiyo Juni mosi mwaka huu akiwa na upungufu wa damu akaongezwa lita mbili za damu na akabaki hospitalini hapo kwa ajili ya uangalizi na uchunguzi zaidi.

‘’Katika uchunguzi uliofanywa na madaktari ilibainika alikuwa na ujauzito wa watoto mapacha na kutokana na hali aliyokuwa nayo alishauriwa kubaki hospitalini hapo mpaka alipojifungua salama watoto wanne wote wa kike kwa wakati mmoja,’’ amesema Nyanguleta.

Watoto hao, wa kwanza alikuwa na uzito wa kilo mbili, wa pili alikuwa na kilo 1.5 wa tatu kilo 2.6 na wa nne alikuwa na uzito wa kilo 2.1 na kwa mujibu wa maelezo ya Nyanguleta, watoto wote walikuwa na afya njema.

Muuguzi huyo amesema, watoto hao wataendelea kubaki hospitalini hapo kuangaliwa kwa karibu wa madaktari kwa kipindi cha miezi minne.

Huo ni uzazi wa tatu wa mama huyo tangu alipojifungua mtoto wake wa kwanza wa kike mwaka 2004, uzazi wa pili alijifungua watoto mapacha wawili wa kiume na huo wa tatu watoto wanne na kufanya idadi ya watoto saba.

‘’Kwanza namshukuru Mungu kuniwezesha kujifungua watoto wote saba salama na wakiwa hai na kutokana na hali ya kiuchumi ya familia yetu mimi na mume wangu tulikubaliana nifunge kizazi ili tujiandae kuwalea na kuwasomesha watoto wetu’’ amesema Mlinda.

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Deograthias Hella, alimpongeza mama huyo na kumpa zawadi ya Sh. laki tatu na katoni moja ya sabuni nguo za watoto, nepi, sabuni za kuogea, mafuta na nguo za kumfunika vyote vikiwa na thamani ya Sh. 500,000.

Hella ametoa mwito kwa wale wote watakaoguswa na maisha ya mama huyo kujifungua watoto wanne kwa wakati mmoja, kumsaidia kwa chochote walicho nacho kwa kuwa matunzo na malezi ya mapacha hao wanne kunahitaji uwezo na nguvu ya ziada.

Baba wa watoto hao, Tito Isack (32) amesema, kazi yake ni mkulima na uwezo wa familia yake kuwatunza watoto hao ili waishi na afya nzuri ni mdogo na hasa ikizingatiwa kuwa mama wa watoto alikuwa na upungufu wa damu na watoto wote wanahitaji kunyonya

1 comment:

  1. naomba nambari za simu zao ili nami nichangie chochote kwani nimeguswa sana

    ReplyDelete